BUNGE LAIDHINISHA BAJETI YA WIZARA YA KATIBA NA SHERIA
- Tume ya Utumishi wa Mahakama yatekeleza majukumu yake kwa ufanisi
Na Lydia Churi- Tume ya Utumishi wa Mahakama, Dodoma
Bunge la Tanzania limeidhinisha jumla ya shilingi 687,698,489,000 kwa Wizara ya Katiba na Sheria, Taasisi zake pamoja na Mahakama ya Tanzania ambapo fedha hizo zinatarajiwa kutumika kwa ajili ya Matumizi ya Kawaida na Miradi ya Maendeleo katika mwaka wa fedha wa 2025/2026.
Bunge limeidhinisha kiasi hicho cha fedha baada ya Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Dkt. Damas Ndumbaro kuwasilisha Mpango na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Fedha ya Wizara ya Katiba na Sheria, Taasisi zake pamoja na Mahakama ya Tanzania kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026, jana jijini Dodoma,
Akizungumza wakati wa kuwasilisha Mpango huo, kwa upande wa Tume ya Utumishi wa Mahakama, Waziri Ndumbaro alisema Tume imetekeleza kwa ufanisi jukumu lake la kusimamia watumishi wa Mahakama ya Tanzania katika maeneo ya uteuzi, ajira mpya, kuboresha maslahi ya watumishi pamoja na masuala ya nidhamu na maadili katika kipindi cha Julai 2024 hadi Aprili, 2025
Alisema, katika kipindi hicho, Tume ilimshauri Rais juu ya Uteuzi wa Jaji mmoja (1) wa Mahakama Kuu ya Tanzania na pia iliteua Naibu Wasajili sita (6), Mkurugenzi wa Sheria Mkurugenzi Msaidizi wa TEHAMA na Watendaji wa Mahakama wanne (4).
Aidha, Tume iliajiri watumishi 498 wa Mahakama wa kada mbalimbali. Na kuwathibitisha kwenye Cheo cha Uongozi Msajili Mkuu, Msajili wa Mahakama ya Rufani, Msajili wa Mahakama Kuu, Naibu Wasajili 34, Mtendaji wa Mahakama ya Rufani, Mtendaji wa Mahakama Kuu Divisheni na Watendaji wawili (2) wa Mahakama wa Kanda.
Waziri wa Katiba na Sheria aliliambia Bunge kuwa Tume ya Utumishi wa Mahakama iliwathibitisha kazini jumla ya watumishi 283 wa kada mbalimbali.
Katika kuhakikisha maadili na nidhamu kwa watumishi wa Mahakama yanasimamiwa ipasavyo, Tume ilishughulikia mashauri 27 ya nidhamu na kutolewa uamuzi ambapo kati ya mashauri hayo, saba (7) yaliwahusu Maafisa Mahakama (Mahakimu) na 20 ya watumishi wasio Maafisa Mahakama.
Kuhusu kuimarisha Kamati za Maadili ya Maafisa Mahakama za Miko ana Wilaya, Waziri Ndumbaro alisema Tume inaendelea kusimamia na kuhakikisha kwamba kunakuwepo usimamizi madhubuti wa utekelezaji wa majukumu yao.
Alisema katika kipindi cha Julai, 2024 hadi Aprili, 2025 Tume imeratibu ukaguzi wa Kamati za Maadili ya Maafisa Mahakama katika mikoa sabane ni Arusha, Manyara, Iringa, Pwani, Mtwara, Lindi, Njombe na Ruvuma pamoja na wilaya 49 zilizo ndani ya mikoa hiyo.
Alifafanua kuwa ukaguzi huo ulilenga kutathmini namna Kamati zinavyotekeleza majukumu yake, kutoa ushauri wa kuboresha utendaji, na kupokea maoni kutoka kwa wajumbe wa Kamati, hivyo kuimarisha utendaji wa Kamati na nidhamu katika Mahakama na kuongeza imani ya wananchi katika mfumo wa utoaji haki.
Kwa upande wa utoaji wa Elimu kwa Wananchi kuhusu majukumu ya Tume na uwepo wa Kamati za Maadili za Mikoa na Wilaya, Waziri Ndumbaro aliliambia Bunge kuwa, Tume ya Utumishi wa Mahakama ilitoa elimu kwa Umma katika mikoa ya Manyara, Kigoma, Mbeya, Mwanza, Mtwara, Kagera na Mara.
Alisema katika kipindi cha Julai, 2024 hadi Aprili, 2025, vipindi nane (8) vya redio vilirushwa kupitia redio za kijamii za Manyara FM, Smile FM, TBC, Joy Fm Redio, Morning Star Redio, Safari Fm Redio, Redio Free Africa pamoja na mitandao ya kijamii ya Facebook, Instagram, x (uliojulikana kama Twitter) na Youtube.