Kamati hii imeanzishwa kwa lengo la kuishauri Tume kuhusiana na masula ya watumishi wasio maafisa mahakama yanayohusu ajira, kuthibitishwa kazini, kupandishwa vyeo na nidhamu. Kamati hii imeanzishwa chini ya Kifungu cha 14 (2) cha Sheria ya Usimamizi wa Mahakama Sura ya 237. 

Wajumbe

Kamati ya Ushauri wa Ajira itakuwa na Mwenyekiti na wajumbe wengine tisa ambao watachaguliwa na Tume kama ifuatavyo:

i. Mwenyekiti anayeteuliwa kutoka miongoni mwa watu walioko nje ya Utumishi wa Mahakama;

ii. Maafisa Mahakama wawili wanye nafasi ya uongozi wanaoteuliwa kutoka miongoni mwa Maafisa Mahakama;

iii. Mkuu wa Idara ya Uajiri, Uteuzi, na Uthibitisho kutoka Sekretarieti ya Tume;

iv. Mkuu wa Idara ya Maadili na Nidhamu kutoka Sekretarieti ya Tume;

v. Mjumbe mmoja kutoka Wizara inayohusika na Usimamizi wa Utumishi wa Umma;

vi. Wajumbe wawili kutoka Utumishi wa Mahakama ambao si maafisa mahakama lakini wanashikilia nafasi za usimamizi;

vii. Mjumbe mmoja kutoka Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Tanzania; na

viii. Mkurugenzi wa Usimamizi wa Rasilimali Watu wa Mahakama ambaye atakuwa Katibu.

Sifa za Mwenyekiti na Wajumbe

Mtu anastahili kuwa Mwenyekiti au Mjumbe wa Kamati endapo ana:
i. Ujuzi na maarifa yaliyothibitishwa katika usimamizi wa rasilimali watu na utawala


ii. Uzoefu wa kushika nafasi ya usimamizi kwa angalau miaka mitano;

iii. Ni mtumishi wa umma; na

iv.  Ana umri wa chini ya miaka 57.

Majukumu ya Kamati

Majukumu ya Kamati yatakuwa kama yalivyoainishwa chini ya kifungu cha 14(2) cha Sheria. Majukumu hayo ni kuishauri Tume kuhusu ajira, kuthibitishwa kazini, kupandishwa vyeo na nidhamu kwa watumishi wasio Maafisa Mahakama. Katika kutekeleza majukumu yake, Kamati inapaswa kuzingatia:-

i. Sera ya Usimamizi wa Utumishi wa Umma na Ajira, Kanuni za Utumishi wa Mahakama, Muundo wa Mahakama, na miongozo mingine iliyotolewa na Tume;

ii. Kufanya kazi kwa kufuata misingi ya usawa na uwazi katika uteuzi wa wafanyakazi na kuepuka kuingiliwa na mtu yeyote nje ya Kamati;

iii. Kuheshimu misingi ya fursa sawa kwa wote; na

iv. Kuhakikisha inatumia sheria na taratibu kwa usawa kwa wahusika wote.