JAJI MKUU AWAAPISHA WAJUMBE WA TUME YA UTUMISHI WA MAHAKAMA


 Na Lydia Churi- Tume ya Utumishi wa Mahakama

Jaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania na Mwenyekiti wa Tume ya Utumishi wa Mahakama Mhe. George Masaju leo tarehe 13 Machi, 2026 amewaapisha wajumbe wanne wa Tume ya Utumishi wa Mahakama.

Katika hafla iliyofanyika leo kwenye ofisi za Tume ya Utumishi wa Mahakama jijini Dodoma, Jaji Mkuu amemuapisha Jaji wa Mahakama ya Rufani ya Tanzania Mhe. Gerson Mdemu kuwa Mjumbe wa Tume kufuatia uteuzi uliofanywa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan hivi karibuni.

Aidha, Jaji Mkuu pia amemuapisha Mwanasheria Mkuu wa Serikali Mhe. Hamza Johari kuwa Mjumbe wa Tume ya Utumishi wa Mahakama kufuatia kuteuliwa kwa mara ya pili na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali baada ya Uchaguzi Mkuu wa Rais, Wabunge na Madiwani uliofanyika Oktoba 29, 2025.

Jaji Mkuu pia amewaapisha kwa mara ya pili Mawakili Bahame Tom Nyanduga na Dosca Kemilembe Mutabuzi kuwa Wajumbe wa Tume ya Utumishi wa Mahakama baada ya kumaliza kipindi chao cha miaka mitatu cha kuwa Wajumbe wa Tume na kuteuliwa tena na Rais kushika nafasi hiyo kwa mujibu wa Ibara ya 112  (1) (e) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Tume ya Utumishi wa Mahakama inaundwa na wajumbe wafuatao; Jaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania ambaye ni Mwenyekiti, Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Jaji mmoja wa Mahakama ya Rufani anayeteuliwa na Rais, Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania na Wajumbe wawili wanaoteuliwa na Rais.

Tume ya Utumishi wa Mahakama ni chombo kilichoundwa kwa mujibu wa Ibara ya 112 (1) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 ikisomwa pamoja na Sheria ya Usimamizi wa Mahakama Sura ya 237. Chombo hiki kimeundwa kwa lengo la kusimamia utendaji kazi wa Mahakama ya Tanzania ikiwa ni pamoja na kusimamia Ajira na Nidhamu za Watumishi wa Mahakama.