Sisi ni Nani
Tume ya Utumishi wa Mahakama imeanzishwa kwa mujibu wa Ibara ya 112 (1) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 ikisomwa pamoja na Sheria ya Usimamizi wa Mahakama Sura ya 237.
Kabla ya kutungwa kwa Sheria ya Utumishi wa Mahakama Na. 2 ya mwaka 2005, na sasa Sheria ya Usimamizi wa Mahakama sura ya 237, kulikuwa na Tume mbili zilizokuwa zinashughulikia watumishi wa Mahakama yaani Tume ya Utumishi wa Mahakama iliyokuwa inashughulikia Mahakimu Wakazi na Mahakimu wa Wilaya na Tume maalum ya Utumishi wa Mahakama iliyokuwa inashughulikia Mahakimu wa Mahakama za Mwanzo.
Kwa sasa masuala ya ajira na nidhamu ya Watumishi wa Mahakama yanashughulikiwa na Tume ya Utumishi wa Mahakama. Wajumbe na majukumu ya Tume yameainishwa kwenye Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Sheria ya Usimamizi wa Mahakama sura ya 237.
Katika kutekeleza jukumu la kusimamia maadili ya Maafisa Mahakama, Tume imekasimu Madaraka yake kwa Kamati za Maadili katika ngazi mbali mbali. Kamati hizo zimepewa jukumu la kupeleleza na kuchunguza malalamiko dhidi ya Majaji, Mahakimu, na Watumishi wasio Maafisa Mahakama na kuwasilisha taarifa Tume kwa ajili ya uamuzi.