Kamati ya Maadili ya Maafisa Mahakama ngazi ya Mkoa inashughulikia malalamiko ya kimaadili dhidi ya Mahakimu wanaohudumu kwenye Mahakama za Hakimu Mkazi na Mahakama za Wilaya. Kamati hizi zimeundwa chini ya kifungu cha 50 cha Sheria ya Usimamizi wa Mahakama Sura ya 237.
Wajumbe
i. Mkuu wa Mkoa ambaye ndiye Mwenyekiti wa Kamati,
ii. Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi
iii. Katibu Tawala wa Mkoa (RAS)
iv. Wajumbe wawili walioteuliwa na Mkuu wa Mkoa kutoka miongoni mwa watu mashuhuri katika mikoa, ambao wana uadilifu wa hali ya juu, walio na ufahamu na uwezo ambao ni muhimu katika kushiriki kikamilifu katika utekelezaji wenye ufanisi wa majukumu ya kamati.
v. Maafisa Mahakama wawili wanaoteuliwa na Jaji Mfawidhi.
Aidha, katibu wa kamati hiyo atakuwa:
Mwanasheria wa Serikali wa Mkoa katika Mikoa yenye ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali na kwenye Mikoa isiyo na ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Katibu wa Kamati atakuwa ni Katibu Tawala wa Mkoa (RAS).
Majukumu ya Kamati
i. Kupokea na kupeleleza malalamiko yaliyowasilishwa na wananchi dhidi ya Mahakimu wa Mahakama ya Wilaya au Mahakimu wa Mahakama ya Hakimu Mkazi na kuwasilisha ripoti ya uchunguzi Tume.
ii. Kufanya uchunguzi kuhusu mwenendo wa Hakimu wa Mahakama ya Wilaya au Hakimu wa Mahakama ya Hakimu Mkazi kwa kupewa maelekezo na Jaji Mfawidhi na kuwasilisha ripoti kwake au kuchukua hatua muafaka kwa mujibu wa sheria.
iii. Kutekeleza majukumu mengine kadri ambavyo Jaji Mkuu ataelekeza kwa maandishi kwa Mwenyekiti wa Kamati.