JAJI KIONGOZI AVITAKA VYOMBO VYA HABARI KUANDIKA MAZURI YANAYOFANYWA NA MAHAKAMA
Na Lydia Churi- Tume ya Utumishi wa Mahakama
Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania na Mjumbe wa Tume ya Utumishi wa Mahakama Mhe. Mustapher Siyani amevitaka vyombo vya habari nchini kujenga utamaduni wa kuandika habari zinazohusu mazuri yanayofanywa na Mhimili wa Mahakama ili wananchi wajenge imani na Mhimili huo.
Akizungumza na wadau wa utoaji haki nchini wakati wa Mkutano wa Tume ya Utumishi wa Mahakama na wadau hao mjini Dodoma, Jaji Kiongozi amesema kuna umuhimu mkubwa wa vyombo vya habari kushiriki shughuli za uboreshaji wa huduma za Mahakama kwa kuufikishia Umma taarifa sahihi za mapinduzi ya kihuduma.
“Endeleeni kufichua mapungufu yaliyothibitika dhidi ya Mahakama lakini msiishie hapo, zungumzieni na mazuri pia kuhusu Mahakama ili wananchi wajenge imani na sisi”, alisema Jaji Kiongozi.
Alisema ndani ya Mahakama kuna mifumo imara ya kuwajibishana zikiwemo Kamati za maadili ya Maafisa wa Mahakama ngazi za mikoa na wilaya ambazo ni muhimu wananchi wakazifahamu na kuzitumia kuwasilisha malalamiko yao kuhusu utendaji kazi wa Maafisa wa Mahakama wakiwemo Majaji na Mahakimu.
“Ni watanzania wangapi wanafahamu kuwa Jaji au Hakimu anaweza kufikishwa mbele ya kamati ya maadili na changamorto zake za kimaadili zikasikilizwa na kutolewa uamuzi, na je ni wangapi wanajua uwepo wa kamati hizi za maadili?”, alihoji Jaji Siyani.
Alisema ni mara chache vyombo vya habari vikaripoti kuhusu matendo mazuri yanayofanywa na watumishi wa Mahakama kama vile Mtumishi wa Mahakama kukataa rushwa japokuwa wako watumishi wengi wanafanya hivyo.
Alisema vyombo vya habari havina budi kujenga utamaduni wa kuandika mazuri ili jamii ifahamu kuwa wako watumishi waadilifu, wanaoweza kuaminika na wenye kufanya kazi kwa bidii.
Akizungumzia kasi ya umalizwaji wa mashauri mahakamani, Jaji Kiongozi amewataka wajumbe wa kamati za kusukuma mashauri ngazi za wilaya na mikoa kuhakikisha wanahudhuria vikao vya kamati hizo ili vilete tija iliyotarajiwa. Alisema endapo italazimika wajumbe hao kuwakilishwa basi wawakilishi wao wawe ni wale wenye kutoa maamuzi ndani ya vikao hivyo.
Kuhusu safari ya Mahakama kuelekea matumizi kamili ya TEHAMA, Jaji Kiongozi alisema Mhimili huo umedhamiria kuachana na matumizi ya karatasi ifikapo mwaka 2025, kuongeza uwazi na uwajibikaji kwa kuhakikisha kwamba kasi ya utoaji haki inaimarika kupitia matumizi hayo ya Teknolojia.
Aidha Jaji Siyani aliwashauri wadau wa utoaji haki kujiandaa kuingia kwenye matumizi ya TEHAMA kwa kuweka mipango sawasawa na Mahakama ili wasikwamishe juhudi za Mahakama na pia kusaidia kuondokana na mlundikano wa mashauri mahakamani.
Kwa upande wa Mawakili, Jaji Siyani amewataka kuacha kutumia mbinu za kiufundi kuchelewesha upatikanaji wa haki mahakamani. Amewataka Mawakili hao pia kuwasaidia wadaawa kwa kuwajengea mazingira ya kupatanisha kwa kuwa ni takwa la kikatiba.
Tume ya Utumishi wa Mahakama imemaliza ziara yake katika mkoa wa Dodoma na kuendelea na ziara mkoani Singida. Mkoani Dodoma, wajumbe wa Tume hiyo walikutana na wajumbe wa kamati za Maadili ya Maafisa wa Mahakama ngazi ya Mkoa na wilaya Pamoja na wadau wa utoaji haki.