JAJI KIONGOZI AWATAKA WADAU KUACHA KUVAMIA MAENEO YA MAHAKAMA


Na Lydia Churi- Tume ya Utumishi wa Mahakama-Bukoba

Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Mhe. Mustapher Siyani amewataka wananchi na wadau wengine wa utoaji haki kutoingilia au kuvamia maeneo ya Mahakama kwa kuwa kitendo cha kujitwalia maeneo hayo kinaathiri mipango ya Mahakama ya kusogeza huduma karibu na wananchi.

Akizungumza leo mjini Bukoba wakati wa Mkutano wa Tume na wadau wa utoaji haki, Jaji Kiongozi alisema kuwa jumla ya Mahakama za Mwanzo 29 nchini zinakabiliwa na migogoro kwa wananchi kuvamia maeneo hayo lakini Serikali za maeneo husika huamua kuyagawa kwa sababu mbalimbali.

Jaji Kiongozi ambaye pia ni Kamishna wa Tume ya Utumishi wa Mahakama alisema matarajio ya Tume na Mahakama ni kuona wananchi, Serikali za Vijiji na Kata wanatambua  maeneo ya Mahakama na kuyalinda.

’Nchi yetu ina Tarafa 560 na Kata 3,956, lengo la Mahakama ni kusogeza huduma kwa wananchi kwa kuwa na Mahakama za Mwanzo kwenye kila Tarafa na baadaye kila Kata. Hadi sasa tunazo Mahakama za Mwanzo 946 na kati ya hizo 167 hazifanyi kazi kwa sababu mbalimbali na 212 zinatembelewa”, alifafanua.

Alisema kuwa wananchi takribani 3,010 wanalazimika kufuata huduma za haki kwenye Kata nyingine, hivyo Mahakama na Serikali inafanya juhudi ili malengo ya kuwa na Mahakama kwenye kila Kata yatimie. Alisema kwa mwaka huu, jumla ya majengo 60 ya Mahakama za Mwanzo 60 yanatarajiwa kujengwa nchini kote.

Aidha, Jaji Kiongozi pia amezitaka Taasisi wadau wa Mahakama zinazofanya tafiti kuhusu Mahakama na huduma inazozitoa kuzingatia weledi katika ufanyaji wa tafiti hizo na kuihusisha Mahakama pale inapobidi ili matokeo ya tafiti hizo yawe sahihi na yenye athari chanya zitakazosaidia ujenzi wa taasisi imara inayotoa huduma bora.

”Matokeo ya utafiti yasiyo sahihi au taarifa zinazotolewa za wadau bila utafiti zinaweza kuwa na athari hasi kwa taasisi kama Mahakama, ambayo mtaji wake mkubwa ni imani ya wananchi inaowahudumia”, alisema.

Kuhusu uwepo wa Mawakili vishoka, Jaji Siyani amewataka wadau wote wanaotumia huduma za mawakili kuhakiki Mawakili kwa kutumia mfumo wa e-Wakili kabla ya kuwaajiri. Alisema Mwananchi anaweza kutumia simu janja kwa kuandika  jina la wakili au namba yake ya usajili ili kujiridhisha juu ya uhalali wake.

Aliwataka Mawakili wote nchini kujenga utamaduni wa kutambuana kabla ya kuingia mahakamani kwa kutumia mfumo huo ambao umejengwa na Mahakama kwa manufaa ya wote. Alisema kuwa mfumo huo ukitumika vizuri utaondoa tatizo la watu wasio na sifa za uwakili maarufu kama vishoka kuendelea kuwahujumu wananchi kwa kuwadanganya kuwa ni Mawakili wakati sio.