JAJI MKUU AWATAKA MAJAJI NA MAHAKIMU KUFUNGA MASHAURI YA MIRATHI
Na Lydia Churi-Tume ya Utumishi wa Mahakama
Jaji Mkuu wa Tanzania na Mwenyekiti wa Tume ya Utumishi wa Mahakama Mhe. Prof. Ibrahim Hamis amesema wakati umefika wa Tume hiyo kuwachukulia hatua za kinidhamu Maafisa wa Mahakama wasiotoa tarehe za kufunga mashauri ya Mirathi pamoja na kufuatilia utekelezaji wa amri walizotoa.
Akizungumza na Watumishi wa Mahakama Kanda ya Dodoma katika siku ya kwanza ya ziara ya Tume mkoani humo, Jaji Mkuu amesema Mahakama inakabiliwa na changamoto ya mashauri ya Mirathi kutomalizika kwa wakati hivyo amewataka Majaji na Mahakimu kuhakikisha wanaweka mikakati mbalimbali ya kukabiliana na hali hiyo.
‘Ni jukumu la kisheria kutoa kikomo cha kufunga mashauri yanayohusu masuala ya mirathi hivyo hakuna sababu ya kutotoa tarehe hizo, alisema Jaji Mkuu”
Alisema eneo la mirathi lina changamoto kubwa kwa kuwa ni eneo ambalo familia zinafika mahakamani zikiwa hazina umoja na zenye migogoro iliyoanzia kwenye vikao vya familia. Alisema kinachofanyika ni kuhamishiwa kwa migogoro hiyo mahakamani.
Aidha, amewataka Majaji na Mahakimu Wafawidhi kuwa makini na mashauri yanayohusu mirathi kwa kuwa yana nafasi ya kusababisha wizi, ukiukwaji wa maadili na ujanja mwingi.
Katika hatua nyingine, Jaji Mkuu amesisitiza umuhimu wa Maafisa wa Mahakama kutumia takwimu sahihi katika utekeleza mipango na shughuli mbalimbali za Mahakama.
“Takwimu zinatupa undani wa kujua changamoto zilizopo, kujua mafanikio na zinaweza kutumika katika kufanya uboreshaji wa huduma, na pia zinasaidia kujirekebisha badala ya kusubiri wananchi walalamike”, alisema Prof. Juma.
Tume ya Utumishi wa Mahakama imeanza ziara ya siku nne katika mikoa ya Dodoma na Singida yenye lengo la kutangaza shughuli zinazofanywa na Tume hiyo na pia kutoa elimu kuhusu majukumu yake ya msingi. Katika mkoa wa Dodoma, Makamishna wa Tume wamekutana na wajumbe wa Kamati za Maadili ya Maafisa wa Mahakama wa mkoa wa Dodoma pamoja ma wilaya zake.