JAJI MKUU AWATAKA WANANCHI KUWASILISHA MALALAMIKO BADALA YA KUTUHUMU KWA HISIA
Na Lydia Churi- Tume ya Utumishi wa Mahakama-Singida
Jaji Mkuu wa Tanzania na Mwenyekiti wa Tume ya Utumishi wa Mahakama Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma ametoa rai kwa wananchi kuacha kuwatuhumu watumishi wa Mahakama kujihusisha na vitendo vya rushwa kwa kukisia na badala yake wazitumie kamati za Maadili ya Maafisa wa Mahakama kufikisha malalamiko yanayohusiana na masuala ya maadili.
Akizungumza na wajumbe wa Kamati za Maadili ya Maafisa wa Mahakama ngazi ya mkoa na wilaya jana mkoani Singida, Jaji Mkuu amewataka wananchi kuzitumia kamati hizo zilizopo katika mikoa na wilaya zote nchini kuwasilisha malalamiko yanayohusiana na masuala ya nidhamu na maadili ya watumishi wa Mahakama wakiwemo Mahakimu.
“Uwepo wa kamati hizi ni mfumo shirikishi kwa kuwa Tume peke yake haiwezi kutimiza malengo yake yya kusimamia nidhamu na maadili ya Maafisa wa Mahakama bila msaada wa Kamati za maadili zilizopo nchini”, alisema Jaji Mkuu.
Alisema wajumbe wa Kamati za Maadili ngazi za mikoa na wilaya ni wawakilishi wa kazi za Tume ya Utumishi wa Mahakama na kuwa kamati hizo ni macho na masikio ya Tume katika kufahamu hali ya malalamiko pamoja na nidhamu ya Maafisa wa Mahakama.
Mwenyekiti huyo wa Tume alisema wajumbe wa kamati za maadili wanapotekeleza majukumu yao wanasaidia kujenga imani ya wananchi kwa Mhimili wa Mahakama na katika mfumo mzima wa utoaji haki. Aliongeza kuwa mfumo wa utoaji haki unahitaji watumishi waadilifu wakiwemo Majaji na Mahakimu.
Akizungumzia maboresho yanayoendelea ndani ya Mhimili wa Mahakama, Jaji Mkuu alisema yanasaidia kupunguza vitendo vya ukiukwaji wa maadili kwa watumishi huku akitolea mfano wa matumizi ya Teknolojia ya habari na Mawasiliano (TEHAMA) ambayo yamesaidia kuongeza uwazi katika utekelezaji wa shughuli za Mahakama.
Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Saingida, Peter Serukamba ameishauri Mahakama kutoa mafunzo ya mara kwa mara kuhusu maadili kwa watumishi wake ili kuimarisha suala zima la nidhamu na maadili kwa watumishi.
Aidha, Mkuu huyo wa mkoa pia ameishauri Tume ya Utumishi wa Mahakama kuendelea kutoa elimu kwa wajumbe wa Kamati za Maadili ya Maafisa wa Mahakama ili ziweze kuimarika na kushughulikia malalamiko ya wananchi na kusimamia ipasavyo nidhamu na maadili ya watumishi wa Mahakama.
Tume ya Utumishi wa Mahakama inaendelea na ziara yake katika mkoa wa Singida yenye lengo la kuitangaza na kutoa elimu kwa wajumbe wa Kamati za Maadili ngazi ya mkoa na wilaya na kukutana na wadau wa utoaji haki nchini.