JITIHADA ZA RAIS SAMIA KUTETEA NA KULINDA HAKI NCHINI NI DHAHIRI


Na Mwandishi-Mahakama, Dodoma

Jaji Mkuu na Mwenyekiti wa Tume ya Utumishi wa Mahakama, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma amesema Serikali imefanya jitihada kubwa katika kutetea na kulinda haki na imethibitisha kwa vitendo nia yake ya kuhakikisha kuwa mfumo wa haki nchini unaboreshwa.

Akizungumza katika hafla ya uzinduzi wa Wiki ya Sheria katika Viwanja vya Nyerere Square tarehe 27 Januari, 2024, Jaji Mkuu alisema Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan mara kadhaa ametoa wito wa kuongeza kasi ya upelelezi wa mashauri ya jinai ili kulinda haki za watuhumiwa na amekuwa akisisitiza kufanyika kwa maboresho katika mfumo wa haki jinai ili kutatua changamoto zilizopo. 

“Serikali inayoongozwa na Dkt. Samia Suluhu Hassan imethibitisha kwa vitendo nia yake ya kuhakikisha kuwa mfumo wa haki nchini unaboreshwa kwa kuunda Tume ya Haki Jinai kwa lengo la kupata changamoto za mfumo huo na kutoa mapendekezo,” alisema. 

Mhe. Prof. Juma amebainisha pia kuwa ili kuenzi jitihada zinazofanywa na Serikali, Mahakama imeamua mwaka huu 2024, kukaa pamoja na wadau wa haki jinai kujadiliana nafasi ya kila mmoja katika kuboresha mfumo wa utoaji haki nchini. 

“Pia tunalenga kutumia maadhimisho haya ya Wiki ya Sheria kutoa mrejesho kwa umma kuhusu ni kwa namna gani Mahakama imetekeleza maazimio ya Tume ya Haki Jinai. 

“Katika maonesho haya tumeweka banda moja maalum linalojumuisha wadau wote wa haki jinai ambao kila mmoja wetu atatumia fursa hii kutoa mrejesho kwa umma ni kwa namna gani Taasisi yake imetekeleza mapendekezo ya Tume ya Haki Jinai,” alisema. 

Jaji Mkuu anawaalika wanachi wote kutumia fursa hiyo adhimu kupata mrejesho wa utekelezaji wa mapendekezo ya Tume ya Haki Jinai kutoka kwa wadau wote muhimu kwenye banda moja, jambo ambalo halitakuwa rahisi baada ya kipindi hiki.

Jaji Mkuu ameeleza pia kuwa kwenye nchi ya demokrasia huwezi kuzungumuzia wadau wa haki bila kukitaja chombo chenye mamlaka ya kutunga sheria, yaani Bunge, ambalo ni mlinzi wa haki na hutekeleza hilo kwa kutunga sheria ambazo zinalinda haki za binadamu zilizotamkwa na Katiba pamoja na matamko mbalimbali ya Kimataifa juu ya haki za Binadamu. 

“Natambua kuwa zipo baadhi ya Sheria au vifungu ambavyo Tume ya Haki Jinai ilishauri vifanyiwe marekebisho ili kuboresha mfumo wa haki jinai. Ni matumaini yetu kuwa kufanyika kwa marekebisho ya sheria hizi pamoja na nyingine ambazo zinasababisha changamoto katika mchakato wa haki jinai kutaleta faida ya ustawi wa Tanzania,” amesema.

Mhe. Prof. Juma alisema kauli mbiu ya maadhimihso ya Wiki na Siku ya Sheria mwaka huu 2024 inasema, “Umuhimu wa Dhana ya Haki kwa Ustawi wa Taifa: Nafasi ya Mahakama na Wadau Katika Kuboresha Mfumo Jumuishi wa Haki Jinai."

Alieleza kuwa kauli mbiu hiyo ni sehemu ya usemi kwamba hakuna nchi inayoweza kujitambulisha kuwa ni ya kidemokrasia na utawala bora kama haifuati misingi ya haki, kwani haki ni msingi wa uhuru, udugu, amani na utulivu ambao utatoa nafasi kwa shughuli za kisiasa, kiuchumi na kijamii kufanyika.

Kilele cha Maonesho ya Wiki ya Sheria kitafanyika tarehe 1 Februari, 2024 katika Viwanja vya Chinangali jijini Dodoma ambapo Mgeni Rasmi anatarajiwa kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan.