MKUU WA WILAYA YA SUMBAWANGA KUELIMISHA KUHUSU KAMATI ZA MAADILI


Na Lydia Churi-Tume ya Utumishi wa Mahakama- Rukwa

Mkuu wa wilaya ya Sumbawanga, Bw. Nyakia Ally Chirukile ameahidi kushirikiana na Tume ya Utumishi wa Mahakama katika kuelimisha wananchi kuhusu uwepo wa Kamati za Maadili ya Maafisa Mahakama ngazi za wilaya ili wananchi waweze kupata haki kwa wakati.

Akizungumza na Watumishi wa Sekretariet ya Tume ya Utumishi wa Mahakama leo mjini Sumbawanga, Mkuu huyo wa wilaya alisema kwa kuanzia, atatoa elimu kwa kamati ya Maadili ya Maafisa Mahakama ngazi ya wilaya ambapo yeye ni Mwenyekiti wake.

Alisema endapo Mwananchi atafahamu sehemu sahihi ya kuwasilisha malalamiko yake yanayohusiana na ukiukwaji wa Maadili ya Mahakimu pamoja na watumishi wengine wa Mahakama ataweza kupata haki kwa wakati.

Aidha Bw. Chirukile ameishauri Mahakama ya Tanzania kuwahamisha Mahakimu waliokaa kwenye kituo kimoja cha kazi kwa muda mrefu ili kuwaepusha watumishi hao kuingia au kuingizwa kwenye vitendo vya ukosefu wa nidhamu na maadili kutokana na kuzoea eneo moja.

“Mahakimu wetu siyo wote ni waungwana hivyo naishauri Mahakama kuwahamisha wale waliokaa kwenye kituo kimoja cha kazi kwa muda mrefu kwani kukaa kwenye kituo kimoja kwa zaidi ya miaka mitatu huweza kusababisha wakaingia kwenye vitendo vya ukiukwaji wa maadili”. Alisema Mkuu huyo wa Wilaya.  

Kwa Upande wake, Naibu Katibu wa Tume ya Utumishi wa Mahakama (Nidhamu na Maadili) Bi. Alesia Mbuya alitoa wito kwa Wakuu wa wilaya pamoja na wajumbe wa Kamati za Maadili ya Wilaya za Sumbawanga na Kalambo kutumia nafasi walizonazo kutangaza uwepo wa kamati hizo ili wananchi wafahamu ni wapi watawasilisha malalamiko yao.

Alisema Tume ya Utumishi wa Mahakama imetengeneza Kanuni za Uendeshaji wa Kamati za Maadili ya Maafisa Mahakama ngazi za Mikoa na Wilaya pamoja na Mwongozo ambao kwa kiasi kikubwa vitarahisisha utendaji kazi wa kamati hizo.  

Naye Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimaliwatu wa Tume, Bw. Rickneville Mwanri amewashauri Makatibu Tawala wa wilaya kuzitumia ipasavyo kamati za Maadili ya Maafisa Mahakama katika kusimamia nidhamu na maadili ya Mahakimu wa Mahakama za Mwanzo kwenye maeneo yao.

Alitoa rai kwa viongozi hao kuwafahamisha wananchi kuhusu uwepo wa kamati hizo na namna ya kuwasilisha malalamiko yanayohusu ukiukwaji wa maadili kwa Mahakimu na watumishi wengine wa Mahakama.

Watumishi wa Sekretariet ya Tume ya Utumishi wa Mahakama wanafanya mafunzo kwa wajumbe wa Kamati za Maadili za Mikoa na Wilaya katika mikoa ya Rukwa na Katavi pamoja na wilaya zake kwa lengo la kuwajengea uwezo na kuziimarisha kamati hizo.