MSAJILI MKUU ATOA WITO KWA WANANCHI KUELIMISHANA KUHUSU USULUHISHI


Na Lydia Churi- Tume ya Utumishi wa Mahakama-Dodoma

Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania Mhe. Wilbert Chuma ametoa wito kwa wananchi na wadau wa Mahakama waliopata elimu kuhusu utatuzi wa migogoro kwa njia ya usuluhishi kuwa chachu katika kuwaelimisha wengine umuhimu wa kutatua migogoro kwa njia hiyo mbadala.

Akifunga Maonesho ya wiki ya Sheria katika Viwanja vya Nyerere ‘Square’ jana jijini Dodoma, Msajili Mkuu alisema endapo wananchi na wadau watatumika kama chachu katika kutoa elimu watakuwa wanatekeleza kwa vitendo Kaulimbiu ya wiki ya sheria ya mwaka huu na pia watasaidia kulinda amani na kukuza uchumi wa nchi.  

Kauli mbiu ya wiki ya sheria mwaka huu inasema “Umuhimu wa Utatuzi wa Migogoro kwa Njia ya Usuluhishi katika Kukuza Uchumi Endelevu: Wajibu wa Mahakama na Wadau.”

Mhe. Chuma alisema anaamini kuwa kila Taasisi iliyoshiriki maonesho hayo itakuwa imejipambanua ipasavyo kwenye kauli mbiu kuelimisha wananchi na kuonesha utayari wao wa kusaidia utatuzi wa migogoro kwa njia ya usuluhishi. “Kimsingi, usuluhishi ni takwa la kikatiba na ni kwa mujibu wa ibara ya 107A (2) (d) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,” alisema.

Aidha Msajili Mkuu alizitaja baadhi ya faida za utatuzi wa miogogoro kwa njia ya usuluhishi kuwa ni pamoja kupunguza mlundikano wa mashauri, kuokoa muda wa kusikiliza shauri mahakamani na kulinda amani ya nchi.

Aidha; Msajili Mkuu Mahakama ya Tanzania imeridhishwa na idadi ya Taasisi za wadau wa utoaji haki zilizoshiriki kwenye Maonesho hayo. Jumla ya Taasisi 38 zilishiriki katika maonesho hayo. Aliongeza kuwa mwitikio kwa taasisi hizo unatokana na uhusiano mzuri uliojengeka kati ya Mahakama na wadau hao na  utayari wa wadau hao katika kuelimisha wananchi na kuboresha huduma.

Wiki ya Sheria nchini ilizinduliwa tarehe 22 Januari, 2023 na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Philip Mpango. Aidha, kilele cha Siku ya Sheria nchini kitafanyika Februari Mosi, 2023 katika Viwanja vya Chinangali mkoani Dodoma na Mgeni Rasmi atakuwa ni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan.  

Wadau walioshiriki katika Maonesho hayo ni Tume ya Utumishi ya Mahakama Chama Cha Wanasheria Wanawake (TAWLA), Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), Tume ya Haki za Binadamu, Tume ya Kurekebisha Sheria, Taasisi ya Usuluhishi, Baraza la Ushindani, Ofisi ya Mkemia Mkuu Wa Serikali, Mamlaka ya Kuthibiti Dawa za Kulevya, Kamisheni ya Usuluhishi na Uamuzi, Kituo cha Haki za Binadamu,

Taasisi nyingine zilizoshiriki kwenye maonesho hayo ni Wengine ni Taasisi ya Mafunzo ya Sheria kwa Vitendo, RITA, Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Wizara ya Katiba na Sheria, NMB, TAKUKURU, Wakili Mkuu Wa Serikali, Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari (TPA), Chama Cha Majaji Wanawake (TAWJA), Mahakama ya Afrika Mashariki, Jeshi la Magereza, Ofisi ya Taifa ya Mashtaka, Chuo Cha uongozi wa Mahakama Lushoto, Idara ya Uhamiaji, Wizara ya Ardhi Nyumba Na Maendeleo ya Makazi, Jeshi la Zimamoto, Jeshi La Polisi, Tume ya Taifa ya Uchaguzi, na BRELA.