MWANASHERIA MKUU WA SERIKALI AWATAKA WADAU WA UTOAJI HAKI KUWA WAADILIFU
Na Lydia Churi- Tume ya Utumishi wa Mahakama, Dodoma
Mwanasheria Mkuu wa Serikali na Kamishna wa Tume ya Utumishi wa Mahakama, Mhe. Dkt. Eliezer Mbuki Feleshi amewataka wadau wa utoaji haki nchini kuwa waadilifu wanapotekeleza majukumu yao ya kuwahudumia wananchi.
Akizungumza mara baada ya kutembelea mabanda mbalimbali kwenye Maonesho ya wiki ya Sheria yanayoendelea katika viwanja vya Nyerere Square jijini Dodoma, Dkt. Feleshi alisema Uadilifu, Weledi na Uwajibikaji kama ilivyo salaam inayotumiwa na Mahakama ya Tanzania ni dhana ambayo haikwepeki katika zama hizi na hasa kwenye suala zima la utoaji wa haki.
”Uadilifu ni jambo ambalo kila Mtanzania anapaswa kulibeba na hasa kwa wale wanaofanya kazi za utoaji haki”, alisisitiza Mwanasheria Mkuu wa Serikali na Kamishna wa Tume.
Aidha, Dkt. Feleshi alisema amefurahishwa na uwepo wa banda linalowakutanisha Wadau wa Haki Jinai kwenye Maonesho hayo na kwamba uwepo wa banda hilo ni kwa mara ya kwanza tangu kuanzishwa kwa maadhimisho ya Wiki ya Sheria.
“Mimi ni Mjumbe ya Kamati ya Maboresho ya Mfumo wa haki jinai nakiri kufurahishwa na uwepo wa banda la Wadau wa Haki jinai ambapo nilipowatembelea wote wametoa maelezo ya namna taratibu zinavyotakiwa kuwa, na ni kwa jinsi gani utekelezaji wa mapendekezo ya mfumo wa haki jinai unafanyika,” alisema.
Alisema Maonesho ya Wiki ya Sheria yamekuwa ya mafanikio kwa kuwa kumekuwa na mwitikio mkubwa wa wadau wanaoshiriki katika kutoa elimu. Kamishna huyo wa Tume amewataka wananchi kujitokeza kwa wingi kwenye maonesho hayo ili kupata elimu ya sheria na kuwasilisha malalamiko yao.
“Kwanza napenda kuishukuru Mahakama ya Tanzania kwa kutualika sisi wadau wake kushiriki katika maonesho haya, napenda pia kukiri kuwa mwitikio wa wadau katika maonesho haya ni mkubwa, hivyo nitoe rai kwa wananchi wenye malalamiko kujitokeza,” alisema.
Katika hatua nyingine, Mwanasheria Mkuu wa Serikali ameipongeza Mahakama kwa kuzindua Mfumo wa Unukuzi na Tafsiri (TTS) ambapo alisema mfumo huo utasaidia kuwapunguzia Majaji na Mahakimu kazi kubwa wanayofanya ya kuandika na kuwezesha uamuzi kwa haraka zaidi. Aliongeza kuwa mfumo huo pia utaongeza uwazi na kupunguza malalamiko.
Maonesho ya Wiki ya Sheria yanaendelea hadi tarehe 30 Januari, 2024 na kilele cha Siku ya Sheria kitafanyika tarehe 01 Februari, 2024 ambapo Mgeni Rasmi anatarajiwa kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan.