RAIS SAMIA AWAAPISHA MAKAMISHNA TUME YA UTUMISHI WA MAHAKAMA


Na Mwandishi- Tume ya Utumishi wa Mahakama

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan tarehe 10 Februari, 2023 amewaapisha wajumbe wapya wa Tume ya Utumishi wa Mahakama walioteuliwa hivi karibuni.

Hafla hiyo ya kuwaapisha viongozi hao wapya ilifanyika katika Ikulu ya Chamwino jijini Dodoma na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali wa Serikali, Bunge na Mahakama ya Tanzania, akiwemo Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma.

Wajumbe hao wapya walioapishwa ni Jaji wa Mahakama ya Rufani ya Tanzania, Mhe. Dkt. Gerald Ndika, ambaye anaendelea na wadhifa huo na Mawakili wawili wa Kujitegemea, Mhe. Tom Nyanduga na Mhe. Docas Mutabuzi.

Mawakili hao wawili wanachukua nafasi ya Makamishna waliomaliza muda wao wa kuitumikia Tume ya Utumishi wa Mahakama ambao ni Wakili Kalolo Bundala na Wakili Genoveva Kato.

Tume ya Utumishi wa Mahakama imeundwa na wajumbe ambao Jaji Mkuu wa Tanzania, Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Jaji mmoja wa Mahakama ya Rufani anayeteuliwa na Rais, Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania na wajumbe wawili wanaoteuliwa na Rais.   

Majukumu ya Tume yameelezwa kwenye Ibara ya 113 (1) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ikisomwa pamoja na kifungu cha 29 cha Sheria ya Uendeshaji wa Mahakama Na. 4 ya mwaka 2011.

Tume ya Utumishi wa Mahakama imeundwa na Ibara ya 112 (1) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977. Aidha, Tume hii ni chombo cha kikatiba kilichopewa jukumu la kusimamia uendeshaji wa Mahakama ya Tanzania.