RC SHINYANGA AIPONGEZA TUME KWA KUIMARISHA KAMATI ZA MAADILI


Na Lydia Churi- Tume ya Utumishi wa Mahakama

Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Maadili ya Maafisa Mahakama mkoani humo Mhe. Mboni Mhita ameipongeza Tume ya Utumishi wa Mahakama kwa juhudi zake katika kusimamia na kuimarisha nidhamu, uwajibikaji na maadili kwa Watumishi wa Mahakama ya Tanzania.

Akifungua mafunzo ya siku mbili kwa wajumbe wa Kamati za Maadili ya Maafisa Mahakama za Mkoa wa Shinyanga pamoja na wilaya zake jana mkoani humo, Mkuu wa Mkoa alisema mafunzo hayo ni ya msingi na muhimu kwa kuwa yatasaidia kuwajengea uwezo wajumbe wa Kamati za Maadili kutekeleza majukumu yao kwa haki, weledi na kwa uadilifu.  

Alisema mafunzo hayo ni muhimu kwa wajumbe wa Kamati za Maadili kwa kuwa yatawasaidia wajumbe kufahamu kanuni, miongozo na taratibu za uendeshaji wa kamati hizo ili watende haki na kuwa na maadili. Aliongeza kuwa maadili  bora ni nguzo  ya haki na msingi wa imani ya wananchi kwa Mhimili wa Mahakama.

”Bila maadili thabiti, heshima na hadhi ya Mahakama hubakia mashakani, hivyo jitihada za Tume ya Utumishi wa Mahakama zinapaswa kuungwa mkono na wadau wote wa haki”, alisisitiza. 

Mkuu wa Mkoa alisema Serikali mkoani Shinyanga itaendelea kushirikiana na Tume na Mahakama katika kuhakikisha wananchi wanapata haki kwa wakati na kwa usawa.

Awali akimkaribisha Mkuu wa Mkoa kufungua mafunzo, Jaji wa Mahakama kuu ya Tanzania kanda ya Shinyanga Mhe. Ruth Masamu alisema ushiriki wa Wajumbe wa Kamati za Maadili ya Maafisa Mahakama kwenye mafunzo hayo ni kielelezo cha utayari wao katika kuimarisha maadili ya utumishi wa Mahakama na jamii kwa ujumla.

”Uwepo wenu leo hapa unaonesha dhamira yenu ya dhati ya kusimamia maadili, nidhamu na uwajibikaji wa Mahakimu katika maeneo yenu ya kazi”, alisema Jaji Masamu.

Sekretariet ya Tume ya Utumishi wa Mahakama imeandaa mafunzo ya siku mbili kwa Wajumbe wa Kamati za Maadili ya Maafisa Mahakama Mkoa wa Shinyanga pamoja na wilaya zake kwa lengo la kuwajengea uwezo katika uendeshaji wa Kamati hizo kwa ufanisi.