WAJUMBE KAMATI ZA MAADILI WAAHIDI KUTENDA HAKI
Na Lydia Churi- Tume ya Utumishi wa Mahakama, Shinyanga
Mkuu wa Wilaya ya Kishapu Bw. Peter Masindi ameihakikishia Sekretarieti ya Tume ya Utumishi wa Mahakama kuwa Kamati za Maadili ya Maafisa Mahakama za Mkoa wa Shinyanga pamoja na wilaya zake zitatenda haki zitapotekeleza jukumu lake la msingi la usimamizi wa maadili na nidhamu ya Mahakimu.
Akifunga mafunzo ya siku mbili kwa Wajumbe wa Kamati za Maadili ya Maafisa Mahakama, kwa niaba ya Katibu Tawala wa mkoa huo tarehe 20 Agosti, 2025, Bw. Masindi alisema mafunzo hayo yamewawezesha wajumbe wa kamati hizo kufahamu kwa kina majukumu yao katika kusimamia maadili na nidhamu za Mahakimu kwenye maeneo yao.
”Kwa kuwa kazi yetu kubwa inahusisha haki za watu, tutajitahidi sana kufanya kazi kwa umakini na weledi wa hali ya juu na kuhakikisha tunatunza siri za kamati kulingana na viapo vyetu”, alisema Mkuu huyo wa Wilaya.
Kuhusu vikao vya Kamati, Mkuu huyo wa Wilaya alisema vikao hivyo vipo kwa mujibu w3a Sheria hivyo watahakikisha vinafanyika nne kwa mwaka kama inavyotakiwa na kuwasilisha taarifa za vikao hivyo kwenye Sekretariet ya Tume ya Utumishi wa Mahakama.
Aidha, aliipongeza Sekretarieti ya Tume ya Utumishi wa Mahakama kwa kuandaa Mafunzo hayo muhimu kwa wajumbe wa Kamati kwa kuwa yatasaidia kwa kiasi kikubwa kuimarisha utendaji kazi wa Kamati za Maadili ya Maafisa Mahakama.
Sekretarieti ya Tume ya Utumishi wa Mahakama iliandaa mafunzo ya siku mbili kwa Wajumbe wa Kamati za Maadili ya Maafisa Mahakama Mkoa wa Shinyanga pamoja na wilaya zake kwa lengo la kuwajengea uwezo wajumbe hao katika uendeshaji wa Kamati hizo kwa ufanisi.