WATUMISHI TUME YA UTUMISHI WA MAHAKAMA WASHIRIKI MICHEZO YA SHIMIWI


Na Lydia Churi-Tume ya Utumishi wa Mahakama-Tanga

Watumishi wa Tume ya Utumishi wa Mahakama ni miongoni mwa watumishi wa Umma 1,000 wanaoshiriki mashindano ya michezo mbalimbali ya Shirikisho la Michezo ya Wizara na Idara za Serikali (SHIMIWI) iliyoanza jana tarehe 1 Oktoba, 2022 jijini Tanga.

Mashindano ya Shimiwi yanatarajiwa kufunguliwa rasmi na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa tarehe 5 Oktoba mwaka huu ambapo kauli Mbiu ya mashindano ya Shimiwi mwaka huu ni "Michezo hupunguza magonjwa yasiyoambukiza na kuongeza tija Mahala pa kazi".

Aidha, Watumishi wa Tume ya Utumishi wa Mahakama watashiriki katika mashindano ya mchezo wa riadha pamoja na michezo ya ndani ikiwemo Karata, Bao, na Drafti. Mashindano ya Shimiwi yanatarawa kumalizika katikati 15, 2022.

Akizungumza kabla ya kuanza kwa mashindano hayo, Mwenyekiti wa Shimiwi Taifa Bw. Daniel Mwalusamba alisema mashindano hayo yatashirikisha michezo ya Mpira wa miguu, Netbali, Kuvuta Kamba Riadha, Karata, Bao, Drafti, kurusha Tufe na kuendesha Baiskeli. Mwenyekiti huyo pia alitumia nafasi hiyo kuwapa wanamichezo hao dondoo muhimu za namna mashindano hayo yatakavyoendeshwa kwa muda wa wiki mbili kwa kuzingatia sheria, kanuni na taratibu za Utumishi wa Umma.

Katika jiji la Tanga, mashindano hayo yanayoshirikisha michezo mbalimbali yatafanyika katika viwanja nane tofauti ambavyo ni pamoja na Mkwawani, Shule ya Sekondari Galanos, shule ya Sekondari Popatlal, Bandari, Polisi Chumbageni, shule ya sekondari Tanga na katika viwanja vya Gymkhana jijini Tanga.

Mashindano ya Shimiwi yanafanyika kwa mara ya 36 tangu kuanzishwa kwa mashindano hayo nchini.