BUNGE LAIDHINISHA SHILINGI BILIONI 441.3 BAJETI YA WIZARA YA KATIBA NA SHERIA NA TAASISI ZAKE


  • Waziri Atoa wito kwa wananchi kuwasilisha Malalamiko Tume

Na Lydia Churi- Tume ya Utumishi wa Mahakama- Dodoma

Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania leo tarehe 29 Aprili, 2024 limeidhinisha kiasi cha shilingi Bilioni 441,260,152,000 ikiwa ni bajeti ya Mwaka wa Fedha 2024/2025 ya utekelezaji wa shughuli mbalimbali ikiwemo Miradi ya Maendeleo ya Wizara ya Katiba na Sheria na Taasisi zilizo chini yake. 

Akizungumza wakati akiwasilisha Hotuba ya Mipango na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara hiyo kwa Mwaka huo wa Fedha Bungeni jijini Dodoma, Waziri wa Katiba na Sheria, Balozi Mhe. Dkt. Pindi Chana (MB) amesema Wizara hiyo imeendelea kusimamia na kuratibu utekelezaji wa mipango inayolenga kufanikisha jukumu la kuimarisha mifumo ya utoaji haki kwa kuweka mazingira yanayohakikisha usawa kwa wote na kwa wakati.

Mhe. Dkt. Chana amesema Serikali kupitia Wizara imejikita kushughulikia masuala manne ili kuhakikisha haki inapatikana kwa wote na kwa wakati. Aliyataja mambo hayo kuwa ni kufanya mapitio ya mfumo wa Haki Jinai na kuandaa mpango wa marekebisho ya Sheria ambazo zinatoa mianya ya ama kuchelewesha upatikanaji wa haki au ukandamizaji katika upatikanaji wa haki.

Akijibu hoja za Wabunge,  Waziri wa Katiba na Sheria ametoa wito kwa watanzania wenye malalamiko yanayohusu ukiukwaji wa maadili kwa Maafisa Mahakama kuwasilisha malalamiko yao kwenye Kamati za Maadili ya Maafisa Mahakama za Mikoa na wilaya.

Alisema Serikali inavyo vyombo imara vya kusimamia nidhamu na maadili ya watumishi wake zikiwemo Kamati za Maadili za Maafisa Mahakama za mikoa na wilaya zilizowekwa kwa mujibu wa Sheria.

“Mashauri ya kinidhamu ya Watumishi wa Mahakama ya Tanzania yanashughulikiwa na Kamati hizi, hivyo wananchi wenye malalamiko msikose kuwasilisha malalamiko yenu kwenye kamati hizi” alisema Waziri huyo.

Akizungumzia uimarishwaji wa Kamati za Maadili ya Maafisa Mahakama, Waziri wa Katiba na Sheria alisema Tume ya Utumishi wa Mahakama imefanikiwa kutoa mafunzo kwa wajumbe 91 wa Kamati za Maadili katika mikoa ya Mbeya na Songwe.

Kuhusu usikilizwaji wa mashauri, Waziri wa Katiba na Sheria alisema Mahakama imeendelea na mpango wa kupunguza mrundikano wa
mashauri mahakamani, katika kipindi cha Julai, 2023 hadi Aprili, 2024 mashauri  196,592 yalishughulikiwa ambapo kati ya mashauri hayo, 133,82 yalisikilizwa na kuhitimishwa na mashauri 62,769 yaliyobaki. Ameongeza kwamba, katika mashauri yanayoendelea kusikilizwa, mashauri ya umri mrefu ni 2,087 pekee sawa na asilimia tatu (3) ya mashauri yote yaliyobaki mahakamani.


Awali akichangia hoja, Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu wa Bunge ya Utawala, Katiba na Sheria, Mhe. Dkt. Joseph Mhagama ameipongeza Wizara ya Katiba na Sheria kwa kufanya Mapinduzi makubwa katika mfumo wa utoaji kupitia Mahakama ya Tanzania pamoja na Taasisi zilizo chini ya wizara hiyo.

“Watanzania sasa wanaona umuhimu na manufaa ya Wizara ya Katiba na Sheria ambayo imekuwa ni nguzo ya amani ya Taifa la Tanzania”, alisema Mbunge huyo.

Aidha, ameipongeza Mahakama kwa ongezeko la miundombinu ya kutolea haki hususan majengo kuanzia yale ya Mahakama za Mwanzo mpaka Mahakama ya Rufani. Mbunge huyo pia ameipongeza Mahakama kwa kuwa na mpango wa kujenga majengo mengi ya Mahakama za Mwanzo ambapo wananchi wengi zaidi watafikiwa na huduma za kimahakama.

Mhe. Mhagama ameipongeza Mahakama kwa kuanzisha Mfumo wa Unukuzi na Tafsiri-TTS utakaoongeza ufanisi zaidi. Ameishauri Mahakama kuusambaza Mfumo huu kwenye majengo yote ya Mahakama nchini ili wananchi wengi zaidi wanufaike. Hivi sasa mfumo huu umefungwa kwenye majengo 11 ya Mahakama nchini.

Bunge limeidhinisha kiasi cha shilingi Bilioni 441,260,152,000 ikiwa ni bajeti ya Mwaka wa Fedha 2024/2025 ya utekelezaji wa shughuli mbalimbali ikiwemo Miradi ya Maendeleo ya Wizara ya Katiba na Sheria na Taasisi zilizo chini yake. Baadhi ya Taasisi hizo ni pamoja na Tume ya Utumishi wa Mahakama, Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora, Mahakama, Tume ya Kurekebisha Sheria, Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali, na Ofisi ya Taifa ya Mashtaka.