RAIS SAMIA AMUAPISHA JAJI MKUU WA TANZANIA


Na Lydia Churi Tume ya Utumishi wa Mahakama- Dodoma

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan leo tarehe 15 Juni, 2025 amemuapisha Mhe. George Mcheche Masaju kuwa Jaji Mkuu wa Tanzania na Mwenyekiti wa Tume ya Utumishi wa Mahakama  katika hafla iliyofanyika Ikulu Chamwino mkoani Dodoma.

Akizungumza katika hafla hiyo, Rais Samia amesema kuwa, matarajio ya Watanzania kwa Jaji Mkuu huyo mpya ni pamoja na kuona kuwa Mahakama inaendelea zaidi ya ilipo sasa na haki inatendeka.

Rais Samia alimtaka Jaji Mkuu kuendeleza yote mazuri yaliyofanywa na mtangulizi wake Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma ikiwemo kujenga majengo ya kisasa, na kuimarisha mifumo na yote iliyopo mahakamani.

Alisema kuwa matarajio ya Watanzania pia ni kuona Mahakama inaendelea kusimamia haki ndani ya nchi na nje ya nchi, hivyo wananchi wanatarajia kuwa jukumu hili kubwa lisimamiwa vyema.

“Katika kusimamia haki, Siku ya Sheria ya mwaka huu nilisema kuwa kazi yenu ni kusimamia haki. Haki ya kutoa haki ni kazi ya Mungu lakini kwa duniani kazi ya haki ni kazi ya Majaji, hivyo ni muhimu kusimamia haki kwa misingi tuliyojiwekea,” amesisitiza Rais Samia.

Ameongeza kuwa, Serikali itafanya kila linalowezekana kuendeleza utendaji kazi   wa Mahakama kama alivyoahidi wakati analihutubia Bunge kwa mara ya kwanza tarehe 22 Aprili, 2021 akisisitiza kuwa, Serikali itaendelea kufanya hivyo ili Mahakama ya Tanzania isimame vizuri na iwe ni moja katika Mihimili yenye hadhi duniani.

Mhe. Dkt. Samia ametoa rai kwa Jaji Mkuu mpya kuendelea na utekelezaji wa mapendekezo yaliyotolewa na Tume ya Haki Jinai.

“Nenda kaangalie ni maeneo gani tumetekeleza na ambayo bado hatujatekeleza na tuone jinsi tutakavyoendelea kuyatekeleza ili haki isimame vyema ndani ya nchi yetu,” amesema Rais Samia huku akiongeza kwa kumpongeza Jaji Mkuu Mstaafu kwa kuhitimisha kazi hiyo bila makandokando.

Akizungumza baada ya uapisho, Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. George Mcheche Masaju amemshukuru Rais Samia kwa kumuamini na kumuona anafaa kushika nafasi hiyo ya kuongoza Mhimili wa Mahakama ya Tanzania.

“Ninachoweza kusema tu mbele yako Mheshimiwa ni kwamba, sisi kazi yetu Mhimili wa Mahakama ni kutoa haki na Katiba katika Ibara ya 107A na B imetueleza kanuni zinazotuongoza na sheria zote zinazotungwa huwa zina mambo matatu zinazungumza maslahi ya haki, maslahi ya umma na maslahi ya Taifa,” amesema Mhe. Masaju.

 Jaji Mkuu amesema kuwa, katika kutoa haki kuna kanuni ambazo ni mwongozo na mojawapo ya kanuni hizo ni kutenda haki kwa watu wote bila kujali hali ya mtu kiuchumi na kijamii lakini pia kuharakisha utoaji haki isipokuwa kama kuna sababu ya msingi lakini pia kutofungwa na masharti ya kiufundi yanayoweza kusababisha haki kutotendeka kwa wakati.

Jaji Mkuu huyo ameeleza kuwa, ataenda kushauriana na viongozi wenzake wa Mahakama ili kuona ni namna gani zaidi ya kuwafikia wananchi kwa kuwa Mahakama imelenga kuwasaidia wananchi (Citizen Centric Justice Service Delivery).

Amesema kuwa ili kuendelea kutoa huduma kwa wananchi, atajadiliana na wenzake kuona uwezekano wa kuwa na huduma za Mahakama ya Rufani kwa kila mkoa ili kurahisisha upatikanaji wa haki.

Hafla hiyo imehudhuriwa na Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Rais wa Umoja wa Mabunge Duniani (IPU), Mhe. Dkt. Tulia Ackson, Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa na Majaji wa Mahakama ya Rufani ya Tanzania.

Wengine waliohudhuria hafla hiyo ni Waziri wa Katiba na Sheria, Mhe. Dkt. Damas Ndumbaro, Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Mustapher Mohamed Siyani, Jaji Mkuu wa Zanzibar, Mhe. Khamis Ramadhan Abdallah, Mawaziri, Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante ole Gabriel, Msajili Mkuu wa Mahakama, Mhe. Eva Kiaki Nkya pamoja na Viongozi wengine wa Mahakama na Serikali.