SERIKALI KUENDELEZA USHIRIKIANO NA MAHAKAMA
Na Selina Mlelwa-Tume ya Utumishi wa Mahakama, Dodoma
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt Samia Suluhu Hassan amesema Serikali itaendeleza ushirikiano na Mahakama ya Tanzania kwa kuiwezesha kutekeleza majukumu yake ipasavyo na kuifanya isimame na kuwa Mhimili wenye hadhi duniani.
Aidha, Rais Samia pia aliwataka wote wenye fikra hasi kuhusu Ushirikiano uliopo kati ya Serikali na Mahakama kuachana na fikra hizo kwakuwa Mahakama haitaweza kufanya kazi yake kama haitashirikiana na Serikali.
Akizungumza mara baada ya kumuapisha Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. George Mcheche Masaju, jana Ikulu mkoani Dodoma, Rais Samia alisisitiza ushirikiano wa Mahakama na Serikali katika kuboresha huduma ya utoaji haki kwa Wananchi kupitia Miundombinu bora, Wafanyakazi na Mifumo.
“ Dola inaundwa na Mihimili mitatu ambayo ni Serikali, Bunge na Mahakama, sasa Mhimili hii ili Dola iende vizuri, ni lazima ishirikiane.”Alisisitiza Rais Samia.
Kwa upande mwingine Rais Samia alimshukuru Jaji Mkuu Mstaafu Mhe. Prof Ibrahim Hamis Juma kwa kazi kubwa aliyofanya katika kuleta mageuzi makubwa ya kiteknolojia, miundondombinu na kiutendaji ndani ya Mhimili wa Mahakama.
“ Umefanya kazi kubwa sana ya kuendeleza na kuleta mageuzi ndani ya Mahakama, pamoja na kushikwa mkono na Serikali lakini uongozi wako thabiti ndiyo uliyoleta mageuzi yale, umeacha historia na ’Legacy’ kubwa, na kutokana na kazi yako umekuza imani ya Watanzania kwa Mahakama yao”
Aidha Mhe. Rais alimpongeza Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. George Mcheche Masaju kwa kuweka historia ya kuwa Jaji Mkuu wa kwanza kuapishwa Wilaya ya Chamwino mkoani Dodoma baada ya Mahakama kuhamia rasmi Jijini Dodoma.
Alisema matarajio ya Watanzania ni kuona Mahakama inaendelea kusimamia utoaji wa haki ndani ya nchi na nje ya nchi.
Tarehe 13 Juni, 2025 Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, alimteua Jaji wa Mahakama ya Rufani Mhe. George Mcheche Masaju kuwa Jaji Mkuu wa Tanzania, kuchukua nafasi ya Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma ambaye amestaafu kwa mujibu wa Sheria.