DC RORYA KUELIMISHA WANANCHI KUHUSU KAMATI ZA MAADILI KUANZIA NGAZI YA TARAFA HADI VITONGOJI
Na Lydia Churi- Tume ya Utumishi wa Mahakama- Rorya Mara
Mkuu wa Wilaya ya Rorya Ndg. Juma Chikoka amesema wilaya yake inakusudia kuwaelimisha wananchi kuhusu uwepo wa Kamati za Maadili ya Maafisa Mahakama na namna ya kuwasilisha malalamiko yao kuanzia ngazi ya Tarafa hadi vitongoji ili waweze kupata haki.
Akizungumza jana wakati wa mafunzo kwa wajumbe wa Kamati ya Maadili ya Maafisa Mahakama ya wilaya ya Rorya yanayotolewa na Sekretariet ya Tume ya Utumishi wa Mahakama, Mkuu huyo wa wilaya alisema anaamini kuwa wanachi watakapoelimishwa watawasilisha malalamiko yao kwa usahihi na kupata haki zao.
“Tutawaandikia barua Maafisa Tarafa, Watendaji wa Kata na mpaka kwenye ngazi ya vijiji na vitongoji ili watoe elimu kwa wananchi kuhusu uwepo wa kamati hizi na wananchi walete malalamiko yao yanayohusu maadili ya Mahakimu”, alisema.
Alisema wananchi wengi wa wilaya ya Rorya hawafahamu uwepo wa Kamati zinazopokea malalamiko yanayohusu ukiukwaji wa maadili ya Maafisa Mahakama na kuwa endapo watazifahamu kamati hizi ni wazi kuwa Kamati yake itapokea malalamiko kutoka kwa wananchi.
Aidha, Ndg. Chikoka alisema atahakikisha kuwa vikao vya Kamati za Maadili vinafanyika kwa mujibu wa sheria na taratibu zilizowekwa licha ya ufinyu wa bajeti za vikao hivyo uliopo. ‘‘Mtarajie kuona mabadiliko makubwa katika wilaya hii ya Rorya”, alisisitiza,
Akizungumzia mfumo wa kielekitroniki unaotarajiwa kuanzishwa na Tume ya Utumishi wa Mahakama hivi karibuni, Ndg. Chikoka alisema mfumo huo utarahisisha utendaji kazi wa Kamati za Maadili na pia utawawezesha Wananchi kuwasilisha malalamiko yao kwa urahisi zaidi. Hivyo ameishauri Tume kuharakisha uanzishwaji wa mfumo huo.
Kuhusu mafunzo, Mkuu wa wilaya ameipongeza Tume kwa kutoa mafunzo kwa wajumbe wa Kamati za Maadili kwa njia ya kuwafuata walipo kwani njia hiyo inawawezesha wajumbe kupata muda wa kutosha kujifunza na pia kupata uelewa mpana zaidi.
Watumishi wa Sekratariet ya Tume ya Utumishi wa Mahakama wanaendelea na kazi ya utoaji wa Elimu kwa Kamati za Maadili ya Maafisa Mahakama za Mikoa na Wilaya katika mikoa ya Mwanza na Mara pamoja na wilaya zake kwa lengo la kuziimarisha Kamatti hizo.
Tume ya Utumishi wa Mahakama ni chombo cha kikatiba kilichopewa jukumu la kusimamia uendeshaji wa Mahakama ya Tanzania. Moja ya jukumu lake ni kusimamia Maadili ya Maafisa Mahakama ili kuhakikisha Mhimili wa Mahakama unatekeleza jukumu lake la msingi na la kikatiba la kutoa haki kwa wananchi.
Jukumu la kusimamia Maadili ya Maafisa Mahakama pamoja na majukumu mengine ya Tume, yameainishwa katika Ibara ya 113 (1) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kifungu cha 29 cha Sheria ya Usimamizi wa Mahakama Sura ya 237.