DC UKEREWE AIPONGEZA TUME YA UTUMISHI WA MAHAKAMA KWA KUTOA ELIMU


Na Lydia Churi- Tume ya Utumishi wa Mahakama- Ukerewe, Mwanza

Mkuu wa Wilaya ya Ukerewe Mhe. Christopher Ngubyagai ameipongeza Tume ya Utumishi wa Mahakama kwa mpango wake wa kutoa elimu kwa Wajumbe wa Kamati za Maadili ya Maafisa Mahakama unaolenga kuwafikia wajumbe hao kwenye maeneo yao.

Akizungumza jana wakati wa utoaji wa elimu kwa Kamati ya Maadili ya Maafisa Mahakama wilaya ya Ukerewe, Mkuu huyo wa wilaya ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Maadili ya Wilaya hiyo alisema njia iliyotumiwa na Tume kuwapatia elimu kwenye eneo lao inasaidia kwa kiasi kikubwa kujenga uelewa mpana zaidi kwa wajumbe.

“Kwa niaba ya Serikali ya wilaya ya Ukerewe, napenda kutoa pongezi za dhati kwa Mwenyekiti wa Tume ya Utumishi wa Mahakama Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma kwa kuwa na wazo la kutoa elimu hii kwa wajumbe wa Kamati na pia kulitekeleza, tumejifunza mengi na kupata uelewa mpana kuhusu Kanuni na Mwongozo wa Uendeshaji wa Kamati hizi”, alisema.

Aidha, Mkuu wa wilaya ya Ukerewe pia aliishukuru Sekretariet ya Tume ya Utumishi wa Mahakama kwa kutekeleza uamuzi wa Tume wa kutembelea Mikoa na Wilaya kutoa Elimu kuhusu utendaji kazi wa Kamati za Maadili kwa kuwafikia wajumbe wa Kamati hizo moja kwa moja kwenye maeneo yao.

Katika hatua nyingine, Mkuu huyo wa Wilaya ameipongeza Tume kwa kuanza kutekeleza majukumu yake kwa kutumia Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) katika Usaili wa Watumishi wa Mahakama na pia kuandaa mfumo utakaorahisisha utendaji kazi wa kamati za Maadili ya Maafisa Mahakama.

Akizungumzia manufaa ya elimu waliyopatiwa, alisema yatawabadilisha wajumbe wa Kamati yake na kuahidi kuwaelimisha wananchi kupitia mikutano ya hadhara ili nao waifahamu Tume na kuitumia katika kutafuta haki zao.

“Wilaya ya Ukerewe wananchi wake bado hawajafahamu zaidi uwepo wa Kamati ya Maadili ya Mahakimu ya wilaya na jinsi gani wataleta malalamiko yao na changamoto wanazokutana nazo kwenye Mahakama za Mwanzo ili waweze kupata haki”, alisema.

Alisema, akiwa Kiongozi na mlezi wa wilaya ya Ukerewe atafanya kazi kwa ushirikiano wa karibu na wajumbe wa Kamati ya Maadili ya wilaya pamoja na Mahakimu na kuwalea ili wananchi wapate haki na pia Serikali iliyoko madarakani iendelee kukubalika na wananchi wake.

Tume ya Utumishi wa Mahakama ni chombo cha kikatiba kilichopewa jukumu la kusimamia uendeshaji wa Mahakama ya Tanzania. Moja ya jukumu lake ni kusimamia Maadili ya Maafisa Mahakama ili kuhakikisha Mhimili wa Mahakama unatekeleza jukumu lake la msingi na la kikatiba la kutoa haki kwa wananchi.

Jukumu la kusimamia Maadili ya Maafisa Mahakama pamoja na majukumu mengine ya Tume, yameainishwa katika Ibara ya 113 (1) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kifungu cha 29 cha Sheria ya Usimamizi wa Mahakama Sura ya 237.