MAHAKAMA NGUZO MUHIMU UTEKELEZAJI DIRA YA TAIFA YA MAENDELEO: DKT. NCHIMBI  


Na Mwandishi- Tume ya Utumishi wa Mahakama, Dodoma

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Emmanuel John Nchimbi amesema kuwa Mahakama ya Tanzania ni Mhimili muhimu katika kuchochea maendeleo na ustawi wa Taifa kupitia utekelezaji wa haki, utawala wa sheria na kulinda misingi ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Mhe. Dkt. Nchimbi ameyasema hayo leo tarehe 02 Februari, 2026 katika Maadhimisho ya Siku ya Sheria nchini, yenye kauli mbiu isemayo Mchango wa Mahakama katika Maendeleo na Ustawi wa Taifa”, yaliyofanyika katika viwanja vya Makao Makuu ya Mahakama ya Tanzania jijini Dodoma.

Mgeni rasmi katika maadhimisho hayo alikuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, ambaye aliwakilishwa na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Akizungumza kwa niaba ya Rais, Mhe. Dkt. Nchimbi alisema Mahakama ina mchango mkubwa katika kufanikisha Dira ya Taifa ya Maendeleo ya 2050 kwa kuendelea kulinda haki, misingi ya Katiba na kuhakikisha migogoro ya kiuchumi, kibiashara na kijamii inatatuliwa kwa haraka na kwa haki.

Aliongeza kuwa Mahakama imekuwa ikijenga imani kwa wananchi na wawekezaji kupitia mifumo thabiti ya kisheria, sambamba na kukuza uwajibikaji, nidhamu katika utumishi wa umma na sekta binafsi, pamoja na kudumisha amani na mshikamano wa kitaifa ambao ni msingi wa maendeleo endelevu.

Mhe. Dkt. Nchimbi alibainisha pia kuwa Mahakama ina wajibu wa kulinda haki za makundi maalum wakiwemo wanawake, watoto na watu wenye mahitaji maalum, pamoja na kuzuia migogoro inayoweza kusababisha mgawanyiko wa kijamii na kisiasa.

Maadhimisho ya Siku ya Sheria nchini yalihudhuriwa na viongozi mbalimbali wa serikali, Viongozi wa Mahakama ya Tanzania, viongozi wa dini, wawakilishi wa vyombo vya ulinzi na usalama,  pamoja na wadau mbalimbali wa sekta ya sheria.

Maadhimisho ya Siku ya Sheria Nchini yamekuwa jukwaa muhimu la kutafakari na kuimarisha nafasi ya Mahakama katika kuhakikisha utawala wa sheria unazingatiwa kama nyenzo ya msingi ya maendeleo na ustawi wa Taifa.