MAHAKAMA YAENDELEZA MAGEUZI YA UTOAJI HAKI NCHINI
Na. Selina Mlewa -Tume ya Utumishi wa Mahakama
Mahakama ya Tanzania imeendelea kuchukua hatua madhubuti za kuimarisha utoaji haki nchini kupitia ujenzi wa Vituo Jumuishi vya Utoaji Haki, matumizi ya teknolojia ya kisasa, uimarishaji wa haki ya dhamana pamoja na ugatuzi wa huduma za Mahakama ya Rufani.
Jaji Mkuu wqa Mahakama ya Tanzania Mhe. George Masaju ameyasema hayo leo tarehe 02 Februari, 2026 wakati wa Maadhimisho ya Siku ya Sheria nchini yaliyofanyika katika viwanja vya Makao Makuu ya Mahakama ya Tanzania Jijini Dodoma.
Akizungumzia jitihada zilizofanywa na Mahakama ili kuimarisha utoaji haki nchini, Jaji Mkuu alisema vituo Jumuishi vya Utoaji Haki nane (8) vimejengwa na vinaendelea kutoa huduma kwa wananchi, huku vingine saba (7) vikiwa katika hatua za mwisho za ukamilishaji.
Alibainisha kuwa vituo vinavyotarajiwa kuanza kutoa huduma ifikapo mwezi Machi 2026 ni Njombe, Katavi, Singida, Pemba, Songwe, Lindi na Songea, hatua inayolenga kusogeza huduma za haki karibu zaidi na wananchi.
Jaji Mkuu alisema sambamba na ujenzi wa vituo hivyo, yapo majengo yanayofanyiwa ukarabati kwa ajili ya kuanzisha Vituo Jumuishi vya utoaji haki kwa mashauri ya Mirathi, Ndoa na Talaka katika Mahakama kuu Kanda za Dodoma pamoja na Mwanza.
Alisema katika kuimarisha usimamizi wa utoaji haki, Mahakama imetunga jumla ya Kanuni 11 katika kipindi cha Juni hadi Desemba 2025, Kanuni hizo zinahusu masuala mbalimbali ikiwemo usimamizi wa mirathi, mashauri ya kikatiba, ulinzi wa mashahidi, haki ya mtuhumiwa kupata vielelezo vya upande wa mashtaka pamoja na matumizi ya mifumo ya kielektroniki katika uwasilishaji wa mashauri mahakamani.
Aidha, Mahakama imeimarisha haki ya dhamana kwa kuhakikisha kuwa dhamana inapatikana katika Mahakama za Mwanzo, Wilaya na Hakimu Mkazi kwa mashauri yote yanayodhaminika kisheria, na kwamba uamuzi wa dhamana utolewe siku hiyo ombi linapowasilishwa. Hatua hiyo imechangia kupunguza msongamano wa wafungwa na mahabusu magerezani pamoja na kuondoa mianya ya rushwa.
Kuhusu matumizi ya teknolojia, Mahakama inaendelea kuimarisha matumizi ya TEHAMA ikiwemo ujenzi ya mfumo unaotumia Akili Unde (Artificial Intelligence) kwa ajili ya kurekodi mwenendo wa mashauri na hukumu, pamoja na kutafsiri na kuandika mazungumzo ya mahakamani kwa wakati halisi. Mfumo huo unatarajiwa kuongeza ufanisi na usahihi wa kumbukumbu za mashauri.
Jaji Mkuu alisema Mahakama pia inaendelea na mkakati wa ugatuzi wa Mahakama ya Rufani, ambapo baadhi ya huduma zitatolewa katika Kanda mbalimbali ikiwemo Dar es Salaam, Arusha, Mwanza, Mbeya na Tabora, hatua itakayosaidia kupunguza gharama na usumbufu kwa wananchi wanaohitaji haki katika ngazi ya juu.
Kwa upande wa uchumi, Mahakama ilieleza kuwa katika mwaka 2025, mashauri ya kiuchumi yaliyosikilizwa yalikuwa na thamani ya zaidi ya Shilingi trilioni 50, fedha ambazo baada ya mashauri kuhitimishwa zilichangia kukuza biashara, uwekezaji na ustawi wa Taifa.
Jaji Masaju alisisitiza kuwa Mahakama ya Tanzania itaendelea kutekeleza Dira yake ya “Haki sawa kwa wote, mapema ipasavyo”, sambamba na Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, kwa kuzingatia misingi ya utawala bora, uwajibikaji, uadilifu na huduma zinazomlenga mwananchi.
Kauli mbiu ya Maadhimisho ya siku ya Sheria ni “Mchango wa Mahakama katika ustawi na maendeleo ya Taifa”, maana yake Mahakama pamoja na wadau wake kutafakari namna ya kudumisha na kuimarisha mchango wao katika ustawi wa wananchi na maendeleo ya Taifa.
Kwa mujibu wa Ibara ya 8(1)(b) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania lengo kuu la Serikali ni ustawi wa wananchi, na kwamba kwa mujibu wa Ibara ya 4 ya Katiba, Serikali inajumuisha Mahakama; hivyo, Mahakama inabeba wajibu wa kikatiba wa kuchangia moja kwa moja katika ustawi na maendeleo ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia utekelezaji wa haki, utawala wa sheria na ulinzi wa haki za msingi za wananchi.

