IMANI YA WANANCHI KWA MHIMILI WA MAHAKAMA INALINDWA NA USAFI WA WATUMISHI
Na Lydia Churi- Tume ya Utumishi wa Mahakama- Arusha
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Arusha Mhe. Ilvin Mugeta amesema kuwa imani ya wananchi kwa Mhimili wa Mahakama inalindwa na usafi wa Mahakimu wanaosimamiwa na Tume ya Utumishi wa Mahakama.
Akifungua Mkutano wa Baraza la Wafanyakazi wa Tume uya Utumishi wa Mahakama leo tarehe 17 Januari, 2025 jijini Arusha, Jaji Mugeta pia amewataka watumishi wa Tume kuwa wasafi zaidi ili waweze kutekeleza ipasavyo jukumu la usimamizi wa Maadili na nidhamu ya watumishi hao.
”Tume inasimamia nidhamu ya watumishi Mahakimu na wasio Mahakimu katika utumishi wa Mahakama, jambo hili linaitofautisha Tume na Taasisi nyingine zote kutokana na unyeti wa kazi ya Uhakimu na utumishi katika Mahakama”, alisema.
Alisema utendaji katika Mahakama unahusu utoaji haki ambao ndiyo nguzo ya amani katika nchi yoyote duniani hivyo aliwataka watumishi wa Tume kuhakikisha muda wote wananchi wana imani na Mahakama ili wazitumie badala ya kujichukulia sheria mkononi.
”Natambua kuwa baadhi ya Watumishi wa Tume wanadhani utumishi katika Tume ni Utumishi wa Umma wa kawaida lakini ukweli ni kwamba Tume inashikilia amani ya nchi hivyo ninawakumbusha wajibu wenu wa kutunza siri hasa zinazohusu masuala ya Uhakimu”, alisisitiza.
Akizungumzia Baraza la Wafanyakazi wa Tume kukutana kwa baraza hilo ni kielelezo cha kuitikia na kutekeleza ipasavyo matakwa ya kisheria, mkataba baina ya Watumishi na mwajiri na tamko la hayati baba wa taifa Mwalimu Julias Kambarage Nyerere la mwaka 1970 kuhusu kuwashirikisha wafanyakazi kufanya maamuzi katika taasisi kupitia mabaraza ya wafanyakazi.
”Kwa kuwa Mkutano huu ni kwa ajili ya kupitia utekelezaji wa bajeti ya Tume kwa nusu mwaka wa fedha wa 2024/2025, niseme kuwa tija huongezeka pale viongozi wa Taasisi na Watumishi wanaposhirikiana kupanga malengo ya maendeleo na mikakati ya kutekeleza mipango hiyo kwa njia ya majadiliano.
Aidha, Jaji Mfawidhi aliwataka watumishi wa Tume kutumia nafasi hiyo kujadiliana kwa uhuru na uwazi ili yapatikane mapendekezo yatakayoisaidia Tume kutekeleza mipango na majukumu yake kwa ufanisi. Aliwataka kuzibaini na kuzitafutia ufumbuzi changamoto zinazotokana na uhalisia wa utekelezaji wa bajeti kwa kipindi husika.
Aidha aliishukuru na kuipongeza Tume kwa kutekeleza ipasavyo jukumu lake la kuajiri, kupandisha vyeo na kuthibitisha kazini Watumishi wa Mahakama kwa kuwa ni stahili kwa kila mtumishi kwa kuzingatia sifa za kimuundo na uwepo wa bajeti.
Awali akizungumza, Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania ambaye pia ni Katibu wa Tume ya Utumishi wa Mahakama Prof. Elisante Ole Gabriel alisema suala la matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) ni miongoni mwa mambo yanayopewa kipaumbele na Tume.
Hivi sasa Tume inaendesha mchakato wa ajira za Watumishi wa Mahakama ya Tanzania kwa kutumia mfumo wa kielekitroniki. Tume imeanza kutumia akili mnemba kuanzia mwaka 2023 na sasa ni taasisi ya kwanza ya Umma katika kutumia Tehama kwenye zoezi la ajira.
Mtendaji Mkuu wa Mahakama ametoa wito kwa Taasisi nyingine za Serikali zinazofanya michakato ya ajira kujifunza kutoka kwa Tume ya Utumishi wa Mahakama kwa kuwa matumizi hayo yanapunguza gharama za usaili kwa waombaji wa ajira na pia linaleta uwazi.
Naye Katibu wa Chama cha Wafanyakazi cha TUGHE Mkoa wa Dar es salaam Bi. Sara Rwezaula ameipongeza Tume kwa kuzingatia na kutekeleza sheria na ushirikishwaji wa wafanyakazi katika mikutano ya baraza la wafanyakazi.