JAJI BANZI ASISITIZA USIMAMIZI WA MAADILI NA UTENDAJI KAZI
Na Ahmed Mbilinyi, Mahakama-Bukoba
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Bukoba, Mhe Immaculata Banzi amewakumbusha Viongozi wa Mahakama katika Kanda hiyo kusimamia kikamilifu maadili ya watumishi sambamba na utendaji kazi.
Mhe. Banzi aliyasema hayo hivi karibuni wakati akiongoza Kikao cha Menejimenti ya Kanda hiyo kilichofanyika katika ukumbi wa Mahakama Kuu Bukoba.
“Kama Viongozi katika maeneo yenu ya kazi ni lazima kusimamia kikamilifu maadili ya watumishi, kwenye kila Wilaya kuna ninyi viongozi Mahakimu Wafawidhi ambao mnaratibu usimamizi wa Mashauri na Maafisa Utumishi au Tawala mnaratibu usimamizi wa watumishi ni wajibu wenu kusimamia masuala hayo,” alisema Jaji Banzi.
Jaji Mfawidhi hiyo alisema kuwa, kutokuwajibika kwa kiongozi wa kituo ni kutokujua taarifa za nidhamu na mienendo mingine ya watumishi walio chini yake pamoja na kushindwa kuchukua hatua.
Katika hatua nyingine, Mhe. Banzi aliwakumbusha pia watumishi wa Kanda hiyo kuendelea na matumizi ya Mfumo wa Kielektroniki wa Uratibu na Usimamizi wa Mashauri (e-CMS) wakati wa usikilizaji wa mashauri pamoja na matumizi ya mifumo mingine ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA).
Katika Kikao hicho taarifa za mashauri na utendaji kazi za Mahakama Kuu Bukoba, Mahakama ya Hakimu Mkazi na Mahakama za Wilaya zote za Mkoa wa Kagera ziliwasilishwa.
Aidha, Jaji Banzi aliwaeleza wajumbe wa Kikao hicho kuhusu umuhimu wa vikao kama hivyo kwa kuwa ni nyenzo muhimu katika utendaji kazi. “Vikao kama hivi ni muhimu katika sehemu zenu za kazi kwa kuwa ni nyenzo kubwa kwa ustawi wa Vituo vyenu,” alisema.
Lengo la kikao hicho lilikuwa ni kupeana taarifa mbalimbali za kiutendaji na kiutumishi, pamoja na kujua hali ya uendeshaji wa mashauri ndani ya Kanda hiyo.
Kikao hicho kilihudhuriwa na Naibu Wasajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Bukoba, Mhe. Amworo Odira na Mhe. Said Mkasiwa, Mtendaji wa Mahakama Kuu Kanda ya Bukoba, Bw. Lothan Simkoko pamoja na watumishi wengine ambao ni wajumbe wa kikao hicho.