JAJI KIONGOZI AHIMIZA WADAU KUZINGATIA SHERIA, MIONGOZO KATIKA UPELELEZI


Na Faustine Kapama– Mahakama, Mtwara

Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Mustapher Siyani amewahimiza wadau mbalimbali katika mnyororo wa utoaji haki nchini, hususani vyombo vya upelelezi kuzingatia sheria, miongozo na taratibu zilizowekwa ili kuwezesha mchakato wa upelelezi na usikilizaji wa mashauri kwenda kwa wakati, hivyo kuepuka kuchelesha utoaji wa haki kwa wananchi.

Mhe. Siyani ametoa rai hiyo leo tarehe 20 Juni 2022 katika siku ya kwanza ya ziara ya Tume ya Utumishi wa Mahakama chini ya Mwenyekiti wake, Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma ambayo inatembelea Mikoa ya Mtwara, Lindi na Ruvuma kuzungumza na watumishi wa Mahakama na wadau mbalimbali na pia kutoa elimu kuhusu kazi zake.

“Tutambue kwamba ziko sheria, miongozo na taratibu zinazoongoza vyombo vya upelelezi kwa lengo la kuwezesha upelelezi kufanyika kwa wakati, weledi na ufanisi mkubwa. Tuhuma za jinai zisizo na ulazima wa kufikishwa mahakamani zichunguzwe kwanza na hatimaye majalada ya upelelezi yawasilishwe ofisi za mashtaka kwa ajili ya uamuzi na hatua za kimashataka,” amesema.

Akizungumza katika mkutano wa Tume hiyo wakati akitoa maelezo mafupi kuhusu matarajio ya Mahakama kwa wadau, Jaji Kiongozi amesema kuwa Jeshi la Polisi, TAKUKURU, Uhamiaji na TANAPA ni washirika na wadau muhimu wa Mahakama katika kutekeleza jukumu lake la msingi la utendaji kazi ambapo umuhimu wao huonekana katika nyanja kadhaa, ikiwemo uanzishwaji wa mashitaka mahakamani na upelelezi wa makosa ya jinai.

“Changamoto kubwa inavyovikabili vyombo hivi ni ucheleweshaji wa kukamilika kwa kwa upelelezi. Changamoto imepelekea matokeo hasi kama vile kuchelewa kumalizika kwa mashauri husika mahakamani, mahabusu katika mashauri yasiyokuwa na dhamana kukaa magerezani kwa muda mrefu, kuongezeka kwa msongamano magerezani na gharama kubwa ya kuwatunza mahabusu magerezani,” alisema.

Amebainisha kuwa hivi karibuni Sheria ya Mwenendo wa Mashauri ya Jinai (Criminal Procedure Act) imefanyiwa marekebisho kupitia mabadiliko ya sheria (Writen Laws (Misc. Amendments) Act No. 1 of 2022) ambayo ni muhimu, mabadiliko ambayo yakizingatiwa na wadau hasa vyombo vya upelelezi yatakuwa mwarobaini wa baadhi ya changamoto alizozianinisha.

Mhe. Siyani ametaja baadhi ya maeneo yanayogusa marekebisho hayo ikiwemo Kifungu cha 4 ambacho kimeongezewa kifungu kidogo cha 3 ambacho kinaeleza kwamba pale ambapo tuhuma inajumuisha taswira ya madai, kiutawala au jinai ni budi nafuu itolewayo kwa njia ya shauri la madai au taratibu za kiutawala zitekelzwe kwanza kabla ya ufunguaji wa shauri la jinai.

Amesema pia Kifungu cha 91(1) kimefanyiwa mabadiliko na kubainisha kwamba pale ambapo upande wa mashtaka utaondoa shauri kwa nolle prosequi, mshitakiwa hataweza kukamatwa na kushitakiwa tena kwa kosa lilelile, isipokuwa tu kama kuna ushahidi wa kutosha dhidi yake na usikilizaji wa shauri utaanza mara moja.

Kufuatia mabadiliko hayo, Jaji Kiongozi amevishauri vyombo vya upelelezi kutumia njia za kisanyansi kukusanya ushahidi thabiti ili kwenda na maendeleo ya karne ya 21, huku akitolea mfano wa matumizi ya ushahidi wa vinasaba vilivyochukuliwa eneo la tukio, utambuzi wa kisayansi wa vielelezo vinavyohusika na makosa ya jinai na huduma inayotolewa na Forensic Bureau Dar es Salaam.

“Sheria imejenga mfumo thabiti katika kushughulikia changamoto zinazotukabili, hasa mlundikano wa mashauri mahakamani na ucheleweshaji wa mchakato wa utoaji haki, changamoto ambazo kwa sehemu kubwa husababishwa na kuchelewa kukamika kwa upelelezi. Tatizo hili litatatuliwa kwa utashi wa kila mmoja wenu kuzingatia sheria na taratibu zilizopo katika utekelezaji wa majukumu yenu,” alishauri Mhe. Siyani.