JAJI KIONGOZI ATAKA WATUMISHI WANAOKIUKA MAADILI KUCHUKULIWA HATUA STAHIKI
Na Mwandishi-Mahakama, Tabora
Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania na Kamishna wa Tume ya Utumishi wa Mahakama, Mhe. Dkt. Mustapher Mohamed Siyani amewataka Viongozi wa Mahakama na Kamati za Maadili kusimamia nidhamu ya watumishi kwa ukamilifu na kuchukua hatua stahiki dhidi ya Watumishi watakaokiuka maadili ya kazi.
Kamishna Dkt. Siyani ameyasema hayo jana tarehe 24 Machi, 2025 katika ziara ya kikazi Mahakama Kuu Kanda ya Tabora alipotembelea Wilaya za Igunga, Nzega na Uyui na kufanya mazungumzo na watumishi wa Mahakama hizo.
’’Fanyeni kazi kwa moyo na kujenga utamaduni wa kujituma katika utendaji, kuweka malengo ya kazi na kuyafikia na kuzingatia viwango vya juu vya maadili katika utendaji kazi, kwa kufanya hivyo mtaimarisha imani ya wananchi kwa Mhimili wa Mahakama”, alisisistiza.
Alisema ni muhimu kwa watumishi wa Mahakama kufanya kazi kwa moyo na kujenga utamaduni wa kujituma katika utendaji wao, kila mtumishi anapaswa kuweka malengo ya kazi ya wazi na kuyafikia kwa ufanisi, huku akizingatia viwango vya juu vya maadili katika utendaji wake.
Alisema kuwa lengo la Mhimili wa Mahakama ni kuhakikisha Mahakama inabaki kuwa chombo cha kuaminika kinachotoa haki kwa usawa na kwa kuzingatia maadili.
Aidha, Jaji Kiongozi pia alikumbusha juu ya umuhimu wa kujenga imani ya wananchi kwa Mahakama, huku akisisitiza kuwa hatua madhubuti zinapaswa kuchukuliwa ili kurejesha imani kwa wananchi ili kuhakikisha utoaji haki unaenda sambamba na wananchi kuiamini Mahakama na mfumo wa mzima wa utoaji haki.
“Ni muhimu sana, tunapaswa kujenga imani ya wananchi kwa Mahakama. Sisi watumishi wa Mahakama lazima tuchukue hatua thabiti ili kurejesha imani hiyo kwa kuhakikisha kwamba utoaji haki unakwenda sambamba na wananchi kuiamini Mahakama pamoja na mfumo mzima wa utoaji haki”, alisisitiza.
Alisema Mahakama inapaswa kuwa ni chombo cha haki kinachozingatia uwazi, usawa na maadili ili wananchi wawe na imani katika mfumo wake wa haki.
Ziara ya Jaji Kiongozi katika kanda ya Tabora inalenga kukagua shughuli za Mahakama, kukutana na watumishi na kuwasikiliza, kutatua changamoto zao, kuwapa motisha sambamba na kuhimiza utekelezaji wa majukumu kwa kuzingatia maadili ya kazi.