JAJI MAGHIMBI AWATAKA WAJUMBE KAMATI ZA MAADILI KUZINGATIA VIAPO VYAO
Na Lydia Churi- Tume ya Utumishi wa Mahakama. Pwani
Jaji Mfawidhhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Dar es salaam Mhe. Salma Maghimbi amewataka Wajumbe wa Kamati za Maadili ya Maafisa Mahakama kutekeleza majukumu yao kwa kuzingatia kiapo walichoapa.
Jaji Maghimbi ameyasema hayo leo tarehe 25 Februari, 2025 wakati akiwaapisha wajumbe wa Kamati za Maadili ya Maafisa Mahakama wa Mkoa wa Pwani pamoja na wilaya zake katika hafla iliyofanyika mjini Kibaha. Hafla hiyo pia iliambatana na mafunzo kwa Kamati hizo yaliyotolewa na Jaji Mfawidhi yenye lengo la kuimarisha utendaji kazi wa kamati hizo.
Walioapishwa ni baadhi ya wajumbe wa Kamati ya Maadili ya Maafisa Mahakama Mkoa wa Pwani pamoja na baadhi ya wajumbe wa Kamati za Maadili wa Wilaya za Kisarawe, Mafia, Bagamoyo na Kibaha.
Aidha, Jaji Mfawidhi aliwataka wajumbe hao kutangaza uwepo wa Kamati hizo zenye jukumu la kupokea malalamiko ya wananchi yanayohusu ukiukwaji wa maadili kwa Mahakimu. Alisema endapo wananchi watafahamu uwepo wa kamati hizo watazitumia kuwasilisha malalamiko yao.
”Zitambulisheni Kamati za Maadili ya Maafisa Mahakama kwa wananchi ili wazifahamu na kuwasilisha malalamiko yao”, alisisitiza Jaji Maghimbi.
Alisema Kamati za maadili ni nyeti kwa kuwa zinalo jukumu la kusimamia maadili na nidhamu ya Mahakimu hivyo alitoa rai kwa wajumbe hao kutekeleza wajibu wao kwa haki pasipokuwa na huba, chuki wala upendeleo.
Awali akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Mkuu wa Wilaya ya Kibaha Mhe. Nickson Simon amewataka wajumbe wa Kamati za Maadili ya Maafisa Mahakama mkoani humo kutekeleza jukumu lao kwa kumtanguliza Mungu ili waweze kutenda haki.
”Msingi wa maadili ni kuwa na hofu ya Mungu, kwa kuwa kazi za kamati hizi msingi wake ni maadili, hamna budi kutekeleza ipasavyo jukumu hili ” alisistiza Mkuu huyo wa Wilaya.
Tume ya Utumishi wa Mahakama ni chombo cha kikatiba kilichopewa jukumu la kusimamia uendeshaji wa Mahakama ya Tanzania. Moja ya jukumu lake ni kusimamia Maadili ya Maafisa Mahakama ili kuhakikisha Mhimili wa Mahakama unatekeleza jukumu lake la msingi na la kikatiba la kutoa haki kwa wananchi.
Jukumu la kusimamia Maadili ya Maafisa Mahakama, pamoja na majukumu mengine ya Tume, yameainishwa katika Ibara ya 113 (1) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kifungu cha 29 cha Sheria ya Usimamizi wa Mahakama Sura ya 237.
Ili kutekeleza jukumu la kusimamia Maadili ya watumishi wa Mahakama ya Tanzania, Tume inazo Kamati zilizoundwa kuisaidia kwenye jukumu hili. Kifungu cha 33 (1) cha Sheria ya Usimamizi wa Mahakama Sura ya 237 kimeiruhusu Tume kukasimu utekelezaji wa majukumu yake kwenye Kamati zilizoundwa chini ya sheria hiyo. Baadhi ya kamati hizo ni Kamati za Maadili ya Maafisa Mahakama za Mikoa na Wilaya.