JAJI MKUU AHIMIZA MABADILIKO KIFIKRA, MTAZAMO KWENYE UTOAJI HAKI NCHINI


Na Mwandishi-Mahakama, Mwanza

Jaji Mkuu wa Tanzania na Mwenyekiti wa Tume ya Utumishi wa Mahakama, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma amewahimiza Majaji Wafawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania kuendeleza mabadiliko ya kifikira na kimtazamo ili uwekezaji mkubwa wa kimaboresho uliofanyika mahakamani ulete matokeo chanya kwenye mchakato mzima wa utoaji haki kwa Wananchi.

Mhe. Prof. Juma ametoa wito huo leo tarehe 17 Machi, 2025 alipokuwa anafungua Kikao cha Mwaka cha Majaji Wafawidhi wa Mahakama Kuu, Kanda na Divisheni, kinachofanyika kwa siku tatu katika Hoteli ya Malaika jijini Mwanza.

‘Maboresho hayawezekani bila mabadiliko makubwa ya kifikra na mitazamo. Msukumo wa kimaboresho ambao unaendelea lazima tuuendeleze. Kasi na uendelevu lazima tuuendeleze,’ Jaji Mkuu amewaambia Majaji hao na Viongozi wengine Waandamizi wa Mahakama ya Tanzania wanaohudhuria Kikao hicho.

Amebainisha kuwa tayari uwekezaji mkubwa umefanywa katika Mfumo wa Tafsiri na Unukuzi, katika Mfumo wa Usimamizi wa Mashauri na usikilizaji wa mashauri kwa njia ya mtandao, hivyo hayo yote hayatadumu kama hawatayaendeleza na wenye uwezo wa kuyaendelea ni wao wenyewe.

Jaji Mkuu alitoa mfano wa mpango mkubwa wa kudijiti nyaraka zote ambazo wanazitumia, ambao mwaka jana au mwaka juzi ulipoanza kwa mara ya kwanza kulikuwepo na msisimko mkubwa.

‘Uwekezaji mkubwa ambao tumeufanya ni lazima tuhakikishe unakuwa endelevu, vinginevyo tutashindwa kuonesha kiasi kikubwa cha uwekezaji tuliofanya umeleta faida gani kubwa,’ Mhe. Prof. Juma amesema.

Amewakumbusha Majaji hao kuwa wanapozungumzia maboresho wanatakiwa kuhakikisha kwamba badala ya kutaja tu uwekezaji mkubwa ambao wameufanya, waeleze pia faida kubwa ambazo wamevuna kutokana uwekezaji huo.

‘Kuna faida nyingi sana ambazo Mwananchi wa kawaida anapata baada ya sisi kuanza kutumia vifaa hivyo vya kisasa katika utoaji haki. Mwananchi hapendi kusikiliza uwekezaji, bali kuona matunda au matokeo ya uwekezaji huo mkubwa,’ Jaji Mkuu amesema.

Awali, akimkaribisha Jaji Mkuu kufungua Mkutano huo, Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Dkt. Mustapher Mohamed Siyani, amewapongeza Majaji Wafawidhi hao kwa mafanikio makubwa ambayo yamepatikana kwani takwimu zinaonesha kuongezeka kwa kasi ya utoaji haki nchini.

‘Bila shaka, kuongezeka kwa kasi ya umalizaji wa mashauri na kupungua kwa idadi ya mshauri ya mlundikano ni jambo la kupongezwa. Nichukue fursa hii kuwapongeza Majaji Wafawidhi kwa niaba ya Watumishi na Wadau wote wa Mahakama kwa mafanikio haya,’ amesma.

Jaji Kiongozi amebainisha kuwa takwimu za mashauri zinaonyesha kwa Mahakama Kuu, wastani wa kukamilika kwa shauri umeendelea kupungua, kutoka siku 381 kwa mwaka 2021 hadi siku 249 mwaka 2024, Mahakama za Hakimu Mkazi siku 187, Mahakama za Wilaya siku 131 na Mahakama za Mwanzo 37.

‘Hii inaleta hoja ya kutafakari upya iwapo muda uliopo wa kutambua mashauri ya mlundikano unapaswa kurekebishwa ili uendane na hali halisi ya mwenendo wa mashauri mahakamani,’ Mhe. Dkt. Siyani amesema.

Aidha, Jaji Kiongozi amebainisha kuwa kuwepo kwa viwango maalum vya mashauri ambavyo Majaji na Mahakimu wanapaswa kumaliza kila mwaka kumechangia kuhakikisha haki inapatikana kwa wakati.

Kadhalika, ameeleza kuwa kwa mwaka 2024, wastani wa muda uliotumika tangu shauri kufunguliwa hadi kukamilika ulikuwa ni siku 78, pungufu ya siku sita kutoka siku 84, ukilinganisha na mwaka 2023.

Aidha, Mhe. Dkt. Siyani amesema idadi ya mashauri ya mlundikano mbele ya Mahakama Kuu na Mahakama za chini yake kwa mwaka 2024 imeendelea kupungua, kwani ni mashauri 451 pekee, sawa na asilimia 1.2 ya mashauri 37,674 yaliyobakia Disemba 2024, ndiyo yalikuwa ya mrundikano.

‘Hii inaonyesha upungufu wa asilimia 2 kutoka 3 kwa mwaka 2023. Mahakama za Watoto na za Mwanzo zilirekodi asilimia 0 ya mashauri yaliyokuwa na mlundikano mwaka 2024,’ Jaji Kiongozi amewaeleza washiriki wa Kikao hicho.

Mbali na kujadili masuala mbalimbali yanayohusu utendaji wa Mahakama, Kikao hicho pia kinatoa fursa ya kujipima na kujitathmini kuhusu utendaji kazi, sambamba na utekelezaji wa Mpango Mkakati, Dira na Dhima ya Mahakama.

Aidha, Majaji wanapata fursa muhimu ya kubadilishana uzoefu kwenye utendaji wa kazi za Mahakama, pamoja na kutambua na kujadili changamoto mbalimbali zinazojitokeza katika Mahakama Kuu na Mahakama za chini yake na hivyo kutafuta majibu kwa changamoto hizo.