WANANCHI WATAKIWA KUZITUMIA KAMATI ZA MAADILI YA MAAFISA MAHAKAMA


Na Lydia Churi- Tume ya Utumishi wa Mahakama, Arusha

Naibu Katibu wa Tume ya Utumishi wa Mahakama (Maadili na Nidhamu) Bi. Alesia Mbuya ametoa wito kwa Wananchi wa Mkoa wa Arusha kuzitumia Kamati za Maadili ya Maafisa ngazi ya Mkoa na Wilaya kuwasilisha malalamiko yanayohusu ukiukwaji wa Maadili ya Maafisa Mahakama.

Akizungumza na Wananchi kupitia kipindi cha Redio kilichorushwa na Radio 5 leo mkoani humo, Naibu Katibu huyo amesema wananchi wenye malalamiko hawana budi kuwasilisha malalamiko yao kwenye ofisi ya Mkuu wa Mkoa na Ofisi za wakuu wa wilaya kwa kuwa kamati hizo zina jukumu la kupokea, kupeleleza na kuchunguza malalamiko ya wananchi.

Alisema malalamiko yote yanapaswa kuwasilishwa kwa maandishi yakiwa na saini ya mlalamikaji na pia yawe na taarifa za kutosha hasa maelezo ya kitendo kilichotendeka na mazingira yake.

Bi. Alesia alisema Mwananchi yeyote mwenye ushahidi hana budi kuwasilisha malalamiko yake ili yashughulikiwe na Tume. Alitaja wengine wanaoweza kuwasilisha malalamiko kuwa ni Afisa Mahakama, Afisa Sheria, Taasisi mbalimbali, Wakala wa Serikali, na Mawakili.

Kuhusu muda wa kuwasilisha malalamiko, Bi. Alesia alisema kuwa Kanuni za Uendeshaji wa Kamati za Maadili ya Maafisa Mahakama za mwaka 2023 zinaelekeza  kuwasilishwa kwa malalamiko kwenye kamati ndani ya kipindi cha miezi sita tangu tukio lilipotokea. Aliongeza kuwa, endapo malalamiko yatawasilishwa baada ya muda huo kupita, hayatashughulikiwa na Kamati.

Akielezea Kamati za Maadili ya Maafisa Mahakama, Bi. Alesia alisema Kamati ya Mkoa  hupokea, kuchunguza,  na kupeleleza malalamiko dhidi ya Mahakimu wanaofanya kazi kwenye Mahakama za Hakimu Mkazi pamoja na Mahakama za Wilaya na kuwasilisha ripoti Tume ya Utumishi wa Mahakama.

Alisema Kamati ya Mkoa huongozwa na Mkuu wa Mkoa (Mwenyekiti) na Katibu wake ni Mwanasheria wa Serikali Mfawidhi katika Mikoa yenye ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali na Mikoa isiyo na Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Katibu huwa ni Katibu Tawala wa Mkoa.

Aliwataja Wajumbe wengine kuwa ni  Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mkoa, Wajumbe wengine wawili, walioteuliwa na Mkuu wa Mkoa kutoka miongoni mwa watu mashuhuri katika Mkoa na Maafisa Mahakama wawili watakaoteuliwa na Jaji Mfawidhi.

Kwa upande wa Kamati za Maadili za Wilaya, Naibu Katibu alisema kamati hizi hushughulikia mamalamiko ya ukiukwaji wa maadili kwa Mahakimu wanaofanya kazi kwenye Mahakama za Mwanzo na kuwasilisha ripoti Tume ya Utumishi wa Mahakama.

Alisema Kamati hii huongozwa na Mkuu wa Wilaya (Mwenyekiti) na Katibu wa Kamati ni  Katibu Tawala wa Wilaya. Aliwataja Wajumbe wengine kuwa ni Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Wilaya, Wajumbe wawili wanaoteuliwa na Mkuu wa Wilaya kutoka katika watu mashuhuri, mmoja wao akiwa ni kiongozi wa dini na Wajumbe wengine wawili wanaoteuliwa na Jaji Mfawidhi ambao ni Maafisa Mahakama.

’’Kutokana na uwepo wa Kamati hizi, nawasihi Wananchi kuzitumia kuwasilisha malalamiko ya ukiukwaji wa Maadili ya Mahakimu kwenye Ofisi ya Mkuu Mkoa kwa Katibu Tawala wa Mkoa na pia kwenye Ofisi za Wakuu wa Wilaya kwa Makatibu Tawala wa Wilaya”, alisisitiza.

Kifungu cha 33 (1) cha Sheria ya Usimamizi wa Mahakama sura ya 237  kimeruhusu Tume ya Utumishi wa Mahakama kukasimu majukumu yake kwa kamati za Maadili ya Maafisa Mahakama ambazo zimeainishwa kwenye kifungu cha 36 cha Sheria hiyo. Hata hivyo, kifungu cha 50 cha Sheria hiyo kinaunda Kamati za Maadili ya Maafisa Mahakama ngazi ya Mkoa na ngazi ya Wilaya.

Tume ya Utumishi wa Mahakama ni chombo kilichoundwa kwa mujibu wa Ibara ya 112 (1) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 ikisomwa pamoja na Sheria ya Usimamizi wa Mahakama sura ya 237. Chombo hiki kiliundwa  kwa lengo la kusimamia Uendeshaji wa Mahakama ya Tanzania.

Aidha, Mamlaka ya Tume ya Utumishi wa Mahakama kama chombo cha kusimamia ajira na nidhamu za Watumishi wa Mahakama yanatokana na Ibara ya 113 (1) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ikisomwa pamoja na kifungu cha 29 (1) cha Sheria ya Usimamizi wa Mahakama Sura ya 237.