MAHAKAMA KUSIMAMIA SHERIA DHIDI YA WAAJIRI WASIOWASILISHA MICHANGO YA WAFANYAKAZI
Na Mwandishi-Mahakama
Jaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania na Mwenyekiti wa Tume ya Utumishi wa Mahakama Mhe. George Mcheche Masaju amesema Mahakama haitasita kusimamia sheria dhidi ya Waajiri wanaokiuka masharti ya Sheria hususan wasiowasilisha michango ya wafanyakazi kwenye mifuko ya Hifadhi ya Jamii.
Akifungua Mkutano wa Tisa wa Kamati ya Utatu (Tripartite Users Committee) uliofanyika kwenye Ukumbi wa mikutano wa PSSSF tarehe 25 Agosti, 2025 jijini Dar es Salaam, Mhe. Masaju alisema tabia ya Waajiri kutowasilisha michango ya wafanyakazi kwenye mifuko ya hifadhi ya jamii husababisha usumbufu kwa Wafanyakazi na pia kufunguliwa kwa mashauri mengi yanayotokana na migogoro ya kazi.
”Ni muhimu kwa Waajiri kuthamini maslahi na ubinadamu wa wafanyakazi wao badala ya kujikita katika kutaka kutengeneza faida pekee”, alisema Jaji Mkuu.
Alisema Mifuko ya Hifadhi ya Jamii ya PSSSF na NSSF ipo kwa ajili ya kuwalinda wafanyakazi wanapofikia uzee au wanapopata majanga kama ulemavu, au hata kwa familia zao baada ya kifo hivyo waajiri kuchelewa kuwasilisha au kutowasilisha kabisa michango ni kosa la kisheria, na ni dhuluma kwa mfanyakazi.
Hata hivyo, Jaji Mkuu amewataka ambao hawajajisajili kwenye kwenye Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF) wajisajili kwa manufaa ya wafanyakazi.
“Waajiri endeleeni kujali maslahi na ubinadamu wa wafanyakazi na sio faida tu mnazopata, nanyi Wakala wa Usalama Mahali pa Kazi (OSHA) ongezeni bidii katika ukaguzi ili kulinda afya za wafanyakazi na waelimisheni watumishi kuhusu sheria ya OSHA, wafanyakazi wapewe mafunzo ya mara kwa mara,” alisisitiza.
Jaji Mkuu amesema kuwa, hivi karibuni Mahakama itarekebisha Kanuni za Uendeshaji wa Sheria ya Madai (Kanuni ya XXXV) ili madai ya NSSF yaweze kusikilizwa na kutolewa uamuzi wa haraka yaani summary proceedings / summary suit, njia ambayo haitumii mlolongo mrefu wa mashauri ya Madai.
Jaji Masaju vilevile ameishauri Mifuko ya Hifadhi kuwasiliana na Mkurugenzi wa Mashtaka kwani kutokulipa michango ya wafanyakazi kunakofanywa na Waajiri kunaweza vilevile katika mazingira fulani kutafsiriwa kukiuka aya ya 10 ya Sheria ya Makosa ya Uhujumu Uchumi [Sura ya 200 Marejeo ya 2023] ambayo inatengeneza kosa la kuisababishia mamlaka husika hasara.
Aidha, Jaji Mkuu ametoa rai pia kwa Wafanyakazi waliopo Serikalini na katika Sekta binafsi kufanya kazi kwa bidii sambamba na kudumisha nidhamu kazini bila kulazimika kusimamiwa au kusukumwa katika utekelezaji wa majukumu yao.
“Heshimuni Sheria ya Usalama kazini na tambueni haki zenu. Watawala msiwakandamize wafanyakazi bila kuwajulisha haki zao, Kwa wafanyakazi; tambueni haki zenu. ulizeni, fuatilieni, hakikisheni kuwa michango yenu inaenda mahali sahihi. Hifadhi ya jamii ni msingi wa utu. Tuendelee kuwa taifa la haki, linalothamini binadamu kabla ya faida,” alisisitiza.
Aidha, Mhe. Masaju ametoa rai kwa Waajiri kuhakikisha wanatekeleza viwango vya usalama kazini kulingana na sheria, kuwapa wafanyakazi mafunzo ya usalama mara kwa mara kuwasiliana, kuheshimu maelekezo ya usalama kazini na kutoa taarifa za ukiukwaji wa usalama kwa usiri na ujasiri na OSHA kwa ukaguzi wa mara kwa mara ili kubaini hatari mapema.
Kadhalika, Jaji Mkuu amempongeza Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Afya na Usalama mahala pa Kazi kwa kuingia mkataba na Mahakama wa kutoa mafunzo ya miaka miwili kwa Maafisa wa Mahakama na wadau wake kote nchini, jambo ambalo linadhihirisha dhamira ya dhati ya Mhhimili wa Mahakama na Serikali katika kuboresha mazingira ya kazi na huduma kwa wananchi.
Jaji Mkuu alimshauri Mtendaji Mkuu wa OSHA kuangalia namna nyingineyo ya kuisaidia Mahakama kwa kuwanunulia vyombo vya usafiri kama pikipiki Mahakimu walioko katika vituo vya mbali, kompyuta mpakato, au kuangalia vilevile kama wanaweza kujenga majengo ya Mahakama.
Katika hafla ya ufunguzi wa Mkutano huo, Jaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, na Mwenyekiti wa Tume ya Utumishi wa Mahakama alikabidhiwa Tuzo Maalum ya kutambua mchango wake na ushirikiano wake katika kukuza mazungumzo ya kijamii na kukuza Haki ya Kazi nchini.