JAJI MKUU ATAKA KASI ZAIDI MATUMIZI YA TEHAMA MAHAKAMANI
- Asema kila mmoja atapimwa mfumo upi ametumia, kwa kiasi gani
Na Waandishi wa Mahakama-Morogoro
Jaji Mkuu wa Tanzania, na Mwenyekiti wa Tume ya Utumishi wa Mahakama, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma amewahimiza Majaji na Mahakimu kote nchini kuongeza kasi ya matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano-TEHAMA- kwenye usikilizaji wa mashauri ili kufanya vizuri zaidi katika utekelezaji wa jukumu la utoaji haki kwa Wananchi.
Mhe. Prof. Juma ametoa wito huo tarehe 15 Aprili, 2025 alipokuwa akifungua Mkutano Mkuu wa Mwaka 2024 wa Chama cha Majaji na Mahakimu Tanzania (JMAT), uliofanyika mwaka huu 2025 katika Hoteli ya Morena mkoani Morogoro.
‘Taarifa ya Msajili Mkuu katika Mkutano wa Baraza la Wafanyakazi wa Mahakama inaonesha kuwa mwaka jana 2024, sisi wanachama wa Chama cha Majaji na Mahakimu Tanzania, tuliweza kumaliza mashauri mengi (mashauri 245,310) zaidi ya yale yaliyopokelewa (mashauri 242, 284),’ alisema.
Jaji Mkuu aliwapongeza wanachama hao kwa mafaniko makubwa katika kutimiza wajibu wao wa kikatiba kama Mamlaka yenye kauli ya Mwisho ya Utoaji Haki katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Hata hivyo, Mhe. Prof. Juma alibainisha kuwa Majaji na Mahakimu bado wanayo nafasi ya kufanya vyema zaidi endapo watajikita katika matumizi ya TEHAMA kwenye usikilizaji wa mashauri.
Aliwakumbusha kuzingatia Waraka No. 1 wa Jaji Mkuu, ambao unaeleza kuwa uongozi utaanza kupima matumizi ya uwekezaji mkubwa ambao umefanyika kwenye mifumo mbalimbali ya TEHAMA.
‘Ni jambo moja kuwekeza kwenye mifumo ya TEHAMA na ni jambo tofauti kabisa kama hatutumii kikamilifu. Fedha nyingi sana zimetumika katika kuwekeza kwenye mifumo hiyo. Sasa umefika wakati tuweze mwisho wa mwaka kujua nani ametumia mfumo upi na kwa kiasi gani ili tuone mapungufu yapo wapi tuweze kuboresha,’ Jaji Mkuu amesema.
Mhe. Prof. Juma alibainisha pia kuwa, kwa kutumia mifumo ya TEHAMA wataweza kuhifadhi data nyingi zaidi zilizosheheni mambo mengi yanayoweza kuwasaidia kujua kinachoendelea.
Alisema kuwa wamefika katika wakati ambao ni tofauti kabisa na wakati mwengine na kwamba uwepo wa Kituo cha Kutolea Taarifa ambacho kinapokea data zote, utasaidia kuchakata taarifa na kuweza kujua ni maeneo gani yanahitaji maboresho.
‘Ninawaomba sana tuongeze nguvu katika matumizi ya TEHAMA, kwa sababu ule Waraka utakuwa unatupima kama Mahakama na mtu mmoja mmoja ili tuweze kujua uwekezaji mkubwa ambao tumefanya kwenye mifumo kama unatoa matunda makubwa. Ninaamini tukijipima tutakuwa na sifa zaidi ya hizi tulizo nazo sasa,’ amesema.
Jaji Mkuu aliwapongeza na kuwashukuru wanachama wote wa Chama cha Majaji na Mahakimu wa Tanzania kwa kuendelea kutimiza wajibu wao wa kutekeleza Dira ya Mahakama ya Tanzania ambayo ni “Haki Sawa kwa Wote kwa Wakati.”
Awali, akizungumza wakati wa ufunguzi wa Mkutano huo, Rais wa JMAT na Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Manyara, Mhe. John Kahyoza aliupongeza uongozi wa Mahakama kwa kurejesha mahusiano mazuri ya Chama hicho na Mahakama ya Tanzania.
‘Sote ni mashahidi wa mahusiano mabaya ambayo yalikuwepo huko nyuma. Wimbi la mahusiano mabaya hayo halikuikumba Tanzania pekee yake, liliikumba Afrika Mashariki, wengine walidiriki kupelekana mahakamani, sisi tusifikie huko,’ alisema.
Aliwaambia wanachama wa JMAT kuwa ni muhimu mahusiano yao na Mahakama kuyalinda na kuyaheshimu kwa manufaa ya wote. Kadhalika, Mhe. Kahyoza aliupongeza uongozi wa Mahakama kwa kuboresha mazingira ya kufanyia kazi, hususan majengo na maslahi kwa ujumla ya wanachama.