UADILIFU MTAJI WA IMANI YA UMMA KWA MAHAKAMA: JAJI KIONGOZI
Na Lydia Churi- Tume ya Utumishi wa Mahakama, Lushoto
Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania na Mwenyekiti wa Kamati ya Maadili ya Maafisa Mahakama Mhe. Dkt. Mustapher Siyani amesema maadili, uwazi na uwajibikaji ni mambo ya muhimu yatakayoimarisha imani ya Umma kwa Mhimili wa Mahakama.
Akifungua Mafunzo ya siku mbili ya Wajumbe wa Kamati ya Maadili ya Maafisa Mahakama leo tarehe 16 Machi, 2026 katika Wilaya ya Lushoto Mkoa wa Tanga, Jaji Kiongozi amesema miongoni mwa mambo ya kipaumbele kwa Mahakama ni kuhakikisha inaendelea kujenga na kuimarisha imani ya umma kwa muhimili huo wenye kauli ya mwisho katika utoaji wa haki nchini.
Alisema lengo kubwa la juhudi za Mahakama katika kuimarisha imani ya umma ni kuifanya Mahakama kuwa Taasisi ya watu na inayowajibika kwa umma (Citizen Centric Judiciary).
“Imani ndio mtaji wa taasisi yoyote inayotoa haki. Ili kuwa na Mahakama inayoaminiwa na umma, masuala ya maadili, uwazi na uwajibikaji ni ya muhimu na hayawezi kuwekwa kando. Kwa ujumla wake, watumishi wa Mahakama, wanayo dhima ya kwanza ya kuwa waadilifu”, alisema Jaji Kiongozi.
Mwenyekiti huyo alisema kuwa imani ya watumiaji wa huduma za Mahakama haijengwi kwa uamuzi wa haki peke yake bali pia kwa tabia nzuri na mwenendo usiotiliwa shaka wa watumishi wa Mahakama wakiwemo Majaji na Mahakimu.
Alisema matarajio ya umma kwa Maafisa Mahakama (Majaji na Mahakimu) ni kuona kuwa wao swanakuwa ni mfano au tafsiri sahihi ya uadilifu, weledi na uwajibikaji.
“Vitu hivi vitatu, vinajenga kwa pamoja dhana nzima ya maadili. Kwa hiyo, ni muhimu Maafisa Mahakama kuwa na kiwango cha juu cha uadilifu kwani huo ndio mtaji wa imani yetu kwa umma”, alisisitiza.
Alisema ili kulinda na kuimarisha maadili kwa Maafisa Mahakama, Kamati ya Maadili ya Maafisa Mahakama haina budi kusimamia na kufuatilia mienendo na tabia za Maafisa hao na pia kuchunguza kwa umakini na weledi wa hali ya juu wao wa utoaji wa uamuzi.
Aliwataka wajumbe hao kujifunza na kuelewa mambo ya msingi ya kazi yao ili waweze kusimamia kikamilifu nidhamu na maadili ya Maafisa Mahakama. Aliongeza kuwa mafanikio yao yatategemea weledi na ufanisi katika uzingatiaji wa taratibu za kupokea malalamiko, kuchunguza tuhuma, kusikiliza na kutoa uamuzi.
Alisema kuwa mafunzo haya ni muhimu kwa wajumbe wa Kamati, kwani yatawajengea uwezo katika utekelezaji wa majukumu yao, na hivyo kuboresha utendaji kazi wa Kamati.
Alisisitiza kuwa jukumu la Kamati ya Maadili ya Maafisa Mahakama si kutoa adhabu pekee, Kamati hii inapaswa pia kuwa, kichocheo cha uadilifu na uwazi ili kuimarisha imani ya umma kwa Mahakama.
Aidha, Jaji Kiongozi ameipongeza Tume ya Utumishi wa Mahakama kwa kuona umuhimu wa kufanyika kwa mafunzo haya na kutaka yawe endelevu na kujumuisha watumishi wote.
Tume ya Utumishi wa Mahakama imeandaa mafunzo ya siku mbili ya Wajumbe wa Kamati ya Maadili ya Maafisa Mahakama ili kuwajengea uwezo wajumbe hao na kuimarisha utendaji kazi wa Kamati hiyo.

