JAJI MKUU ATOA RAI KWA WADAU WA MAHAKAMA KUZINGATIA MAADILI
Na Lydia Churi-Tume ya Utumishi wa Mahakama-Tabora
Jaji Mkuu wa Tanzania na Mwenyekiti wa Tume ya Utumishi wa Mahakama Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma ametoa rai kwa Wadau wa Utoaji haki nchini kutekeleza majukumu yao kwa kuzingatia maadili ili kuendela kutoa huduma bora kwa wananchi.
Akizungumza na katika Mkutano wa Tume na Wadau hao wa utoaji Haki uliofanyika mkoani Tabora, Jaji Mkuu amewataka wadau hao kuzisoma na kuzifahamu kanuni za Maadili zinazowaongoza katika kutekeleza majukumu yao ili waendelee kutoa huduma bora kwa wananchi wanaotafuta haki,
“Kanuni zinasisitiza wakati wote kuhusu uwezo wa kazi, unaweza kuonekana huna maadili ya kazi endapo uwezo wa kufanya kazi utapungua”, alisema Jaji Mkuu
Alisema ili kuongeza uwezo wa kufanya kazi wakati wote, wadau wa utoaji haki hawana budi kujiendeleza ili huduma wanazozitoa zisishuke kiwango. Aliongeza kuwa ni muhimu kujiendeleza hasa katika karne hii ya 21 yenye mageuzi makubwa kwa kuwa elimu ya wengi ilitokana na maudhui ya karne za 18 na 19.
Kuhusu Uboreshaji wa huduma zinazotolewa na Mahakama ya Tanzania, Jaji Mkuu aliwataka wadau hao kuyatangaza matunda yanayotokana na maboresho hayo ili wananchi wafahamu na kuzitumia huduma hizo wanapotafuta haki zao.
Katika hatua nyingine, Wadau wameipongeza Mahakama ya Tanzania kwa kuongeza kasi ya utoaji haki pamoja na ushirikiano mzuri na wadau katika kutekeleza jukumu la msingi la kutoa haki.
Akizungumza wakati wa Mkutano huo, Mkuu wa Magereza Mkoa wa Tabora, Kamishna Msaidizi wa Magereza Vendeline Raphael Tesha alisema kutokana na Mahakama kuongeza kasi ya usikilizaji wa mashauri hivi sasa msongamano wa mahabusu na wafungwa umepungua.
“Tulikuwa na msongamano mkubwa magerezani, mwaka jana tulikuwa na idadi ya wafungwa 1,490 na leo tuna wafungwa 1,250 na uwezo wa gereza ni kuhudumia wafungwa 1,360, naipongeza Mahakama kwa kuongeza kasi ya usikilizaji wa mashauri”, alisema Mkuu huyo wa Magereza.
Tume ya Utumishi wa Mahakama inaendelea na ziara yake katika mkoa wa Tabora. Ziara hiyo ya Tume inalenga kukutana na wajumbe wa Kamati za Maadili ya Maafisa Mahakama ngazi ya mikoa na wilaya ili kuziimarisha kamati hizo na pia kukutana na wadau wa utoaji haki kwa lengo la kuboresha huduma.