JAJI MKUU ATOA RAI UTATUZI WA MIGOGORO KWA NJIA YA USULUHISHI


Na Lydia Churi- Tume ya Utumishi wa Mahakama-Dodoma

Jaji Mkuu wa Tanzania na Mwenyekiti wa Tume ya Utumishi wa Mahakama, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma ametoa rai kwa wananchi na wadau wa Mahakjama kutumia usuluhishi katika utatuzi wa migogoro mbalimbali kwa lengo la kukuza uchumi na kuokoa muda.

Akizungumza katika kilele cha Siku ya Sheria nchini kilichofanyika tarehe 1 Februari, 2023 katika Viwanja vya Chinangali jijini Dodoma, Jaji Mkuu alisema  utatuzi wa migogoro kwa njia ya usuluhishi unafanana na falsafa ya maridhiano, ustahimilivu na mabadiliko ya kujenga upya nchi na kwamba Haki inayopatikana Mahakamani kwa njia ya kawaida inapatikana kwa kupitia ngazi, vituo vingi, mitiririko na misururu ya hatua ambayo huchangia ucheleshwaji na huongeza gharama za kesi.

“Usuluhishi unahimizwa na Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kama njia bora ya kutatua migogoro kwa haraka na kwa gharama nafuu. Mahakama, Wadaawa na Wadau, wanapotumia njia ya Usuluhishi kutatua migogoro, wanakuwa sio tu wanatekeleza maagizo ya Ibara ya 107A (2) (d) ya Katiba ya Tanzania (1977), bali pia wanatekeleza misingi ya haki nyingine stahiki kwa wahusika wa mgogoro, ambayo ni haki kutocheleweshewa haki bila sababu za msingi inayotambuliwa na Ibara ya 107A (2) (b) ya Katiba,” amesisitiza Mhe. Prof. Juma.

Jaji Mkuu amesema kwamba, ingawa Mahakama ya Tanzania katika Wiki na Siku ya Sheria ilichagua kauli mbiu ya kuhimiza Usuluhishi kama njia mbadala wa kutatua migogoro, lakini pia inaunga mkono kauli iliyotolewa na Rais Samia, mapema mara baada ya kuingia madarakani tarehe 18 Machi 2021, ambapo alihimiza mazungumzo, majadiliano na usuluhishi kwenye migogoro ya kisiasa.

Akizungumzia Kituo cha Usuluhishi kilichopo Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Prof. Juma alisema kilianzishwa kwa lengo la uzoefu na ufahamu wa kina kuhusu dhana ya Usuluhishi kisha kutumia uzoefu huo kusaidia kurahisisha na kuharakisha utatuzi wa mashauri ya madai yanayofunguliwa, kwa kuanzia, katika Masjala za Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam na Divisheni ya Ardhi na vilevile kutumia uzoefu uliopatikana kueneza matumizi ya usuluhishi katika ngazi zote za Mahakama nchini.

Mahakama Kuu ya Tanzania, Kituo cha Usuluhishi kilichoanzishwa Julai, 2015 mahsusi kwa ajili ya kusuluhisha mashauri mbalimbali hadi sasa kimepokea jumla mashauri ya usuluhishi 1942, kati ya idadi hiyo jumla ya mashauri 326 yamesuluhishwa na mashauri 20 yamefanikiwa kiasi. 

Aidha, Prof. Juma aliunga mkono hoja ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali Mhe. Dkt. Eliezer Feleshi katika hotuba yake kuwa, anafikiria kuwasilisha pendekezo ya Sheria bungeni ya kulazimisha Mashauri yote kupitia hatua ya usuluhishi kabla ya kuanza kwa usikilizwaji wa shauri husika kwa njia ya kawaida.

Jaji Mkuu alizitaja baadhi ya faida za usuluhishi ambazo ni pamoja na; kusaidia kutatua migogoro kwa haraka ambapo inachukua takribani siku 30 kwa shauri la usuluhishi kukamilika, kuleta amani na mshikamano, kukuza uchumi wa nchi na kadhalika.

Alisema, usuluhishi ni muhimu katika kutatua migogoro ya ardhi kwa kuwa migogoro ya aina hiyo ni adui mkubwa kwa maendeleo, amani na ustawi wa wananchi. Ameongeza kuwa, Sheria ya Mahakama za Ardhi, sura ya 216 inatambua umuhimu wa matumizi ya usuluhishi katika utatuzi wa migogoro ya ardhi inayofikishwa mbele ya Mabaraza ya Ardhi ya Vijiji na kwenye Mabaraza ya Kata.

Kuhusu kuimarisha utendaji kazi wa Mahakama, Jaji Mkuu alimshukuru Rais Samia kwa kuteua Majaji 22 mwezi Agosti, mwaka jana ili kuongeza nguvu kazi na hivyo kupunguza mzigo wa mashauri kutoka 340 hadi 265 kwa kipindi hicho. Amekiri kuwa, idadi hiyo imeongeza kasi ya usikilizwaji wa mashauri kutoka asilimia 112 kwa mwaka 2021 hadi kufikia asilimia 113 kwa mwaka jana.

Mbali na uteuzi wa Majaji, Jaji Mkuu alimshukuru Rais kwa fursa ya ajira ya watumishi wapya 292 wakiwemo Mahakimu Wakazi 48, kukamilisha ujenzi wa Majengo mapya 32, Serikali kuridhia na kufanikisha kuingia katika makubaliano na  Benki ya Dunia ya kuongeza fedha na muda wa utekelezaji wa Mradi wa Maboresho.