JAJI MKUU ATOA RAI WADAU KUANDAA KANUNI ZA MAADILI


Na Lydia Churi- Mahakama

Jaji Mkuu wa Tanzania ambaye pia ni Mwenyekiti wa Tume ya Utumishi wa Mahakama Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma amewaomba wadau mbalimbali wa Mahakama kujitengenezea utaratibu wa kutangaza kanuni zao za maadili ili kuongeza uwazi na uwajibikaji wa watumishi kwa wananchi katika mnyororo mzima wa utoaji haki.

Akizungumza katika Mkutano wa Tume hiyo na wadau wa utoaji haki leo mjini Songea, Jaji Mkuu alisema Mahakama ya Tanzania imejiwekea utaratibu wa wazi wa kushughulikia maadili ya watumishi na kupokea malalamiko ya wananchi yanayohusiana na maadili.

“Sisi hatuogopi kukosolewa na hatusiti kupokea malalamiko kwa sababu malalamiko hayo yanaweza kuleta kiu kwa wananchi ya kutaka kujua zaidi shughuli zinazofanywa na Mahakama”, alisema Jaji Mkuu.

Jaji Mkuu pia amewaomba wadau hao wa Mahakama kutangaza namna wanavyoshughulikia malalamiko ya kimaadili yanayoelekezwa kwao na wananchi ili watanzania wengi zaidi wafahamu na kuwasilisha malalamiko yao. Alisema, hatua itasaidia upatikanaji wa haki kwa wakati.

Alisema malalamiko dhidi ya Mahakama hutokana na shughuli mbalimbali zinazofanywa na wadau wa Mahakama. Alisema kwa mfano malalamiko dhidi ya Madalali wa Mahakama, ni rahisi kwa mwananchi wa kawaida kujua kuwa yanatokana na Mahakama wakati kiuhalisia malalamiko hayo hutokana na kazi zinazofanywa na wadau.

Aidha, Jaji Mkuu pia amewataka wadau wa utoaji haki nchini kutangaza utayari wao wa kupokea malalamiko yanayohusu maadili yasiyofaa kwa watumishi wanaofanya kazi na Taasisi za wadau wa Mahakama wakiwemo Polisi, Magereza, Waendesha Mashtaka, Mawakili wa kujitegemea pamoja na wadau wengine.

Akizungumzia Mawakili, Jaji Mkuu alisema hivi sasa kuna mabadiliko ya sheria yaliyoruhusu Mawakili kuanza kutumika katika Mahakama za Mwanzo nchini hivyo aliwataka wadau kuhakikisha Mawakili hao wanakuwa waadilifu kwa kuwa Mahakama hizo zinabeba asilimia 70 ya mashauri yote.

“Chama cha Wanasheria nchini (Tanganyika Law Society) kianze sasa kushughulikia maadili ya Mawakili wao wenyewe bila vyombo vingine kuwaingilia”, alisisitiza Jaji Mkuu.

Wajumbe wa Tume ya Utumishi wa Mahakama wamemaliza ziara yao yenye lengo la kuitangaza Tume na kuimarisha utendaji kazi wa Kamati za Maadili katika mikoa ya Mtwara, Lindi na Ruvuma. Katika ziara hiyo, Wajumbe hao walikutana na wajumbe wa Kamati za Maadili ya Maafisa wa Mahakama ngazi ya mikoa na wilaya pamoja na wadau wa utoaji haki nchini.

Tume ya Utumishi wa Mahakama imeundwa na Ibara ya 112 (1) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977. Aidha, majukumu ya Tume yameelezwa kwenye katiba hiyo katika Ibara ya 113 (1) ikisomwa pamoja na kifungu cha 29 cha Sheria ya Uendeshaji wa Mahakama Na. 4 ya mwaka 2011. Tume ya Utumishi wa Mahakama ni chombo cha Kikatiba kilichopewa jukumu la kusimamia uendeshaji wa Mahakama ya Tanzania.