JAJI MKUU NA MWENYEKITI WA TUME ATUNUKIWA NISHANI  


JAJI MKUU NA MWENYEKITI WA TUME ATUNUKIWA NISHANI  

Na Waandishi- Mahakama Dodoma

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan amemtunuku Jaji Mkuu wa Tanzania na Mwenyekiti wa Tume ya Utumishi wa Mahakama, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma, Nishani ya Kumbukumbu ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar Daraja la Pili kutokana na kutambua mchango wake kwa Taifa la Tanzania.

Hafla ya kutunuku nishani hizo ilifanyika tarehe 26 Aprili, 2025 katika Ikulu ya Chamwino jijini Dodoma na kuhudhuriwa na Viongozi mbalimbali wa kitaifa wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar.

Walikuwepo pia Viongozi Wakuu wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Baraza la Wawakilishi Zanzibar na Mahakama ya Tanzania na Mahkama ya Zanzibar, Majaji wa Mahakama ya Rufani, Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania na Majaji wengine pamoja na Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania.

Akimtunuku nishani hiyo Jaji Mkuu, Rais Samia alisema, ‘Kwa kutambua mchango wako katika Taifa la Tanzania na utumishi wako, mimi Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania nakutunuku Nishani ya Kumbukumbu ya Muungano Daraja la Pili.’

Viongozi wengine waliotunukiwa nishani kwenye hafla hiyo ni Makamu wa Rais Mstaafu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Ali Mohamed Shein na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Mhe. Balozi Seif Ali Iddi.

Wengine ni Waziri Mkuu Mstaafu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Hayati Edward Ngoyai Lowassa, Waziri Mkuu Mstaafu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Mizengo Kayanza Peter Pinda na Spika Mstaafu wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar, Mhe. Pandu Ameir Kificho.

Viongozi wengine waliotunukiwa nishani hizo ni Katibu Mkuu Kiongozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Hayati Balozi John William Kijazi na Makamu wa Mwenyekiti Mstaafu wa Chama cha Mapinduzi, Mhe. Phillip Mangula, ambaye alitunukiwa Nishani ya Kumbukumbu ya Muungano Daraja la Tatu.

Wasifu wa Mhe. Prof. Juma uliosomwa kwenye hafla hiyo unaonesha kuwa amepata elimu ya Msingi, Sekondani na Vyuo Vikuu katika nchi mbalimbali, ikiwemo Tanzania, Uingereza, Sweden na Ubelgiji.

Amekuwa Mwanachama wa Chama cha Mawakili Tanganyika, Wakili wa Serikali, Kaimu Mkurugenzi wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu na Mjumbe wa Kamati mbalimbali, ikiwemo iliyochunguza mauaji ya Wafanyabiasha wa Madini Mahenge, Morogoro-maarufu Tume ya Jaji Kipenka, Tume ya Kurekebisha Sheria Tanzania na Tume ya Utumishi wa Mahakama.

Kadhalika, Mhe. Prof. Juma amekuwa Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Jaji wa Mahakama ya Rufani Tanzania, Kaimu Jaji Mkuu na baadaye kuwa Jaji Mkuu wa Tanzania, nafasi anayoihudumu hadi sasa.

Mhe. Prof. Juma ameandika vitabu 18 vyenye maudhuri tofauti ya kisheria, amekuwa Mhadhiri katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Kitivo cha Sheria kwa miaka mingi na kwa nyakati tofauti amewahi kufanya kazi za ushauri elekezi-consultancy- kwenye maeneo tofauti nane chini ya Wizara mbalimbali.

Utoaji wa nishani hizo kwa Viongozi mbalimbali ni sehemu ya Maadhimisho ya Miaka 61 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar uliozaa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.