JENGO LA TUME LAKAMILIKA KWA ZAIDI YA ASILIMIA 98


  • Kukabidhiwa Rasmi jijini Dodoma

Na Lydia Churi- Tume ya Utumishi wa Mahakama, Dodoma

Jengo la ofisi za Tume ya Utumishi wa Mahakama linalojengwa jijini Dodoma linatarajiwa kukabidhiwa rasmi kwa Tume Jumamosi tarehe 30 Novemba, 2024 baada ya ujenzi wake kukamilika kwa zaidi ya asilimia 98.

Mkandarasi wa jengo hilo ambaye ni Kampuni ya CRJE (EAST AFRICA) LTD anatarajiwa kukabidhi jengo hilo kwa Tume ya Utumishi wa Mahakama baada ya ukaguzi wa mwisho kufanyika leo jijini humo.

Jengo hilo la Ofisi za Tume linajengwa kwenye kiwanja namba 3 Block D katika eneo la NCC, pembeni ya jengo la Makao Makuu ya Mahakama ya Tanzania.

Aidha kiwanja kilichotumika kujenga jengo hilo kina ukubwa wa mita za mraba 9,590, na kina hati yenye namba DOM008194 iliyotolewa tarehe 22 Julai, 2022.

Akielezea gharama za ujenzi wa jengo hilo, Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Ununuzi na Ugavi cha Tume ya Utumishi wa Mahakama Bi. Bertha Mberesero amesema jengo hilo limegharimu kiasi cha shilingi Bilioni 14.3 (14,300,000,000) na Mzabuni wa jengo hilo ni CRJE (EAST AFRICA) LTD.

Kujengwa kwa jengo la Ofisi za Tume ya Utumishi wa Mahakama jijini Dodoma kunaweka historia kwa Taasisi hiyo kumiliki jengo lake la ofisi tangu kuanzishwa kwake.   

Tume ya Utumishi wa Mahakama ni chombo cha kikatiba kilichopewa jukumu la kusimamia uendeshaji wa Mahakama ya Tanzania. Tume hii imeundwa na Ibara ya 112 (1) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977. Aidha, majukumu ya Tume yameelezwa kwenye katiba hiyo katika Ibara ya 113 (1) ikisomwa pamoja na kifungu cha 29 cha Sheria ya Usimamizi wa Mahakama Sura ya 237.