KAMATI YA MAADILI WILAYA YA KARATU YAKUSUDIA KUTOA ELIMU NGAZI YA KATA NA VIJIJI


Na Lydia Churi- Tume ya Utumishi wa Mahakama- Arusha

Kamati ya Maadili ya Maafisa Mahakama ya Wilaya ya Karatu inakusudia kutoa elimu kwa Watendaji wa Kata na Watendaji wa Vijijini ili nao wakawaelimishe wananchi namna ya kuwasilisha malalamiko yanayohusu ukiukwaji wa maadili ya Maafisa Mahakama pamoja na yale yanayohusiana na suala zima la upatikanaji wa haki.

Katibu Tawala wa Wilaya ya Karatu ambaye pia ni Katibu wa Kamati ya Maadili ya Maafisa Mahakama wa wilaya hiyo Dkt. Lameck Karanga amebainisha hayo wakati alipokuwa akizungumza na Maafisa wa Sekretaeti ya Tume ya Utumishi wa Mahakama hivi karibuni jijini Arusha.

’’Wajumbe wa Kamati ya Maadili ya Wilaya yetu, baada ya kupatiwa Elimu na Tume ya Utumishi wa Mahakama Mwezi Julai tumekubaliana sasa kushusaha elimu hiyo kwa Maafisa Tarafa ambao hupokea malalamiko ya wananchi kwa niaba ya Mkuu wa Wilaya pamoja na Watendaji wa Kata na Vijijini ili wasaidie kuelimisha wananchi”, alisema.

Alisema katika kutekeleza hilo, Wajumbe wa Kamati hiyo ya Maadili ya wilaya wanaandaa Semina ya siku mbili kwa Watendaji wa Kata 14,  Watendaji wa Vijiji 57 na Watoaji wa elimu ya Sheria ili kuwaelimisha namna ya kupokea malalamiko ya wananchi yakiwemo yale yanayohusu ukiukwaji wa Maadili kwa Maafisa Mahakama ili nao wakawaelimishe wananchi.

Akizungumzia uhai wa Kamati ya Maadili ya Maafisa Mahakama Wilaya ya Karatu, Dkt. Karanga alisema wajumbe wa Kamati hiyo tayari wameapishwa kutekeleza jukumu la Msingi la usimamizi wa Maadili ya Maafisa Mahakama na wamekuwa wakikutana kwa mujibu wa Sheria.

Aidha, Sekretarieti ya Tume ya Utumishi wa Mahakama kupitia Kitengo chake cha  Mipango, ufuatiliaji na Tathmini imefanya tathmini ya Utendaji kazi wa Kamati za Maadili ya Maafisa Mahakama katika Mikoa ya Arusha na Kilimanjaro pamoja na baadhi ya wilaya za Mikoa hiyo kwa lengo la kuona namna Kamati hizo  zinavyotekeleza jukumu lake na pia kufahamu changamoto mbalimbali za Kamati hizo.

Watumishi hao wa Tume walifanikiwa kukutana na kufanya mazungumzo na Wanasheria wa Serikali Wafawidhi wa Mikoa ya Arusha na Kilimanjaro ambao ndiyo Makatibu wa Kamati za Maadili za Mikoa hiyo pamoja na Makatibu Tawala wa baadhi ya Wilaya za Mikoa hiyo ambao ndiyo Makatibu wa Kamati za Maadili za Wilaya.

Wilaya zilizotembelewa na Watumishi wa Sekretariti ya Tume ya Utumishi wa Mahakama ni pamoja na Arumeru, Karatu, Arusha Mjini na Monduli kwa Mkoa wa Arusha na Wilaya za Rombo, Hai na Moshi mjini kwa Mkoa wa Kilimanjaro.

Tume ya Utumishi wa Mahakama ni chombo cha kikatiba kilichopewa jukumu la kusimamia uendeshaji wa Mahakama ya Tanzania. Moja ya jukumu lake ni kusimamia Maadili ya Maafisa Mahakama ili kuhakikisha Mhimili wa Mahakama unatekeleza jukumu lake la msingi na la kikatiba la kutoa haki kwa wananchi. 

Jukumu la kusimamia Maadili ya Maafisa Mahakama, pamoja na majukumu mengine ya Tume, yameainishwa katika Ibara ya 113 (1) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kifungu cha 29 cha Sheria ya Usimamizi wa Mahakama Sura ya 237. 

Ili kutekeleza jukumu la kusimamia Maadili ya watumishi wa Mahakama ya Tanzania, Tume inazo Kamati zilizoundwa kuisaidia jukumu hili. Kifungu cha 33 (1) cha Sheria ya Usimamizi wa Mahakama Namba 4 Sura ya 237 kimeiruhusu Tume kukasimu utekelezaji wa majukumu yake kwenye Kamati zilizoundwa chini ya sheria hiyo. Baadhi ya kamati hizo ni Kamati za Maadili ya Maafisa Mahakama za Mikoa na Wilaya.