KAMATI YA MAADILI WILAYANI TUNDURU KUTOA ELIMU KWA WANANCHI


  • Jaji Mfawidhi Songea awaapisha Wajumbe wa Kamati

Na Lydia Churi-Tume ya Utumishi wa Mahakama, Tunduru Ruvuma

Mkuu wa Wilaya ya Tunduru Bw. Simon Chacha amesema wajumbe wa Kamati ya Maadili ya Maafisa Mahakama wilaya ya Tunduru wanakusudia kuwaelimisha wananchi kuhusu uwepo wa Kamati hiyo ili waitumie kupata haki.

Akizungumza wakati wa Mafunzo ya wajumbe wa Kamati ya Maadili ya Maafisa Mahakama ya wilaya ya Tundurru tarehe 11 Februari 2025, Mkuu wa wilaya amesema wananchi wakifahamu uwepo wa Kamati hiyo wataitumia kuwasilisha malalamiko yao yanayohusu ukiukwaji wa Maadili ya Mahakimu.

“Ni lazima tupeleke habari ya uwepo wa Kamati ya maadili kwa wananchi kwa kutumia njia mbalimbali hususan kupitia viongozi walio karibu zaidi na wananchi kama vile Watendaji wa Vijiji, Kata na Tarafa,” alisema Bw. Chacha.

Mkuu wa Wilaya ameipongeza Sekretariet ya Tume ya Utumishi wa Mahakama kwa kuandaa mafunzo ya namna ya kuendesha Kamati za Maadili ya Maafisa Mahakama ambayo yataimarisha utendaji kazi wa wajumbe ambao tayari wameapishwa ili kutekeleza jukumu la kusimamia maadili na nidhamu ya Mahakimu.

Aidha, kabla ya kuanza kwa mafunzo hayo, Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Songea Mhe. James Karayemaha aliwaapisha baadhi ya wajumbe wa Kamati hiyo.

Walioapishwa ni pamoja na Mkuu wa Wilaya ya Tunduru Bw. SimonChacha, Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya ya Tunduru, Mahakimu wengine wawili wanaoteuliwa na Jaji Mfawidhi pamoja na Wajuimbe wengine wawili wanaoteuliwa na Mkuu wa Wilaya ambapo mmoja ni kiongozi wa Dini.

Wakati huo huo, Naibu Katibu (Maadili na Nidhamu) wa Tume ya Utumishi wa Mahakama Bi. Alesia Alex Mbuya alitoia wito kwa Mwenyeviti wa Kamati za Maadili ya Maafisa Mahakama ngazi za mikoa na wilaya kujenga utamaduni wa kukabidhiana  vitendea kazi vya kamati inapotokea Uhamisho au vinginevyo ili kuwe na muendelezo wa utekelezaji wa kazi za Kamati.

Aidha, Naibu Katibu pia ametoa wito kwa wajumbe wa Kamati za Maadili ya Maafisa Mahakama kufanya vikao vya Kamati hizo kwa kuwa vikao hivyo viko kwa mujibu wa Sheria. Vikao vya kamati za Maadili hutakiwa kufanyika mara nne kwa mwaka kwa mujibu wa Sheria.

Alisema Kifungu cha 33 (1) cha Sheria ya Usimamizi wa Mahakama Namba 4 Sura ya 237 kimeiruhusu Tume kukasimu utekelezaji wa majukumu yake kwenye Kamati zilizoundwa chini ya sheria hiyo ambapo Kamati za Maadili ya Maafisa Mahakama za Mikoa na Wilaya ni mojawapo.

Alisema kukutana kwa wajumbe wa Kamati mara nne kwa mwaka kama ilivyopangwa kutasaidia Kamati kutekeleza majukumu yake ipasavyo na kutoa haki kwa wakati. Alifafanua kuwa endapo Kamati itakuwa na shauri la kushughulikia haina budi kulikamilisha ndani ya siku 90 zilizowekwa kisheria na endapo kutakuwa na haja ya kuongeza muda, Jaji Mfawidhi ataongeza siku zisizozidi 30.

Ili kutekeleza jukumu la kusimamia Maadili ya watumishi wa Mahakama ya Tanzania, Tume inazo Kamati zilizoundwa kuisaidia kwenye jukumu hili. Kifungu cha 33 (1) cha Sheria ya Usimamizi wa Mahakama Namba 4 Sura ya 237 kimeiruhusu Tume kukasimu utekelezaji wa majukumu yake kwenye Kamati zilizoundwa chini ya sheria hiyo. Baadhi ya kamati hizo ni Kamati za Maadili ya Maafisa Mahakama za Mikoa na Wilaya.

Tume ya Utumishi wa Mahakama ni chombo cha kikatiba kilichopewa jukumu la kusimamia uendeshaji wa Mahakama ya Tanzania. Moja ya jukumu lake ni kusimamia Maadili ya Maafisa Mahakama ili kuhakikisha Mhimili wa Mahakama unatekeleza jukumu lake la msingi na la kikatiba la kutoa haki kwa wananchi. 

Jukumu la kusimamia Maadili ya Maafisa Mahakama, pamoja na majukumu mengine ya Tume, yameainishwa katika Ibara ya 113 (1) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kifungu cha 29 cha Sheria ya Usimamizi wa Mahakama Sura ya 237.