KAMATI ZA MAADILI ZATAKIWA KUSIMAMIA SHERIA KANUNI NA MIONGOZO INAYOTOLEWA NA TUME


Na Lydia Churi- Tume ya Utumishi wa Mahakama, Mbeya

Mkuu wa Mkoa wa Songwe Dr. Francis Kasabubu amewataka wajumbe wa Kamati za Maadili ya Maafisa Mahakama mkoani humo kusimamia Sheria, kanuni, na miongozo inayotolewa na Tume ya Utumishi wa Mahakama wanapotekeleza mashauri ya nidhamu kwa Maafisa Mahakama ngazi za mikoa na wilaya.

Akifungua Mafunzo ya siku tatu kwa wajumbe wa Kamati za Maadili ya Maafisa Mahakama wa mikoa ya Mbeya na Songwe yenye lengo la kuzijengea uwezo kamati hizo, Dr. Kasabubu amesema endapo Sheria, kanuni na miongozo itazingatiwa ni wazi kuwa wajumbe hao watatekeleza kwa usahihi mashauri ya nidhamu kwa Maafisa Mahakama.

Mkuu huyo wa Mkoa ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Maadili ya Maafisa Mahakama Mkoa wa Songwe alisema mafunzo hayo yanayotolewa na Tume ya Utumishi wa Mahakama yatasaidia kuwajengea uwezo wajumbe wa Kamati za Maadili na kutatua changamoto zilizopo katika utekelezaji wa Sheria, kanuni, taratibu na miongozo ya Utumishi wa Umma.

”Mafunzo haya ni moja ya misingi ya utekelezaji wa utawala bora wa Tume ya Utumishi wa Mahakama inayozingatia Sheria, kanuni, taratibu na miongozo katika usimamizi wa majukumu ya Kamati za Maadili ya Maafisa Mahakama” alisema.

Mkuu huyo wa Mkoa aliwakumbusha wajumbe wa Kamati za Maadili wajibu wao muhimu wa kuhakikisha kuwa haki za Maafisa Mahakama zinalindwa pale inapotokea wamekiuka utaratibu katika utekelezaji wa majukumu yao ya utoaji haki na si kuwakomoa.

Akizungumzia mafunzo hayo, Dr. Kasabubu alisema baadhi ya mada zitakazotolewa kwenye mafunzo hayo ni kuhusu historia ya Tume ya Utumishi wa Mahakama, uwasilishwaji wa malalamiko ya wananchi kwenye Kamati za Maadili na utaratibu wa kuyashughjulikia malalamiko hayo.

Kwa upande wake, Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania kanda ya Mbeya Mhe. Dunstan Ndunguru amewataka wajumbe wa Kamati za Maadili kuyatumia mafunzo hayo kama chachu katika kushughulikia mashauri ya kinidhamu kwa Maafisa Mahakama.

”Naishukuru Tume ya Utumishi wa Mahakama na kuipongeza kwa  kuandaa mafunzo haya muhimu, naamini mafunzo haya yatakuwa ni  endelevu kwa kuwa wajumbe wake wamekuwa wakihama mara kwa mara vituo vyao vya kazi na wengine kuteuliwa wapya hususan wakuu wa Mikoa na wakuu wa Wilaya”, alisema.

Baada ya kukamilika kwa mapitio ya Sheria ya Usimamizi wa Mahakama Namba 4 ya mwaka 2011 sura ya 237 ambazo ni kanuni za Uendeshaji wa Kamati za Maadili ya Maafisa Mahakama wa Mikoa na Wilaya za mwaka 2023, Tume imeanza kutoa mafunzo kwa wajumbe wa kamati za Maadili ili kuboresha utendaji kazi wa Kamati hizo.

Aidha, katika mwaka wa fedha wa 2023/2024, Tume imepanga kufanya mafunzo katika mikoa sita nchini ambayo ni Mbeya, Songwe, Iringa, Njombe, Manyara na Arusha.