KAMISHNA WA TUME AWATAKA MAWAKILI KUTOKUWA KIKWAZO KWENYE USULUHISHI


Na Lydia Churi-Tume ya Utumishi wa Mahakama, Dodoma

Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, ambaye pia ni Kamishna wa Tume ya Utumishi wa Mahakama Mhe. Mustapher Siyani amewataka Mawakili wa Kujitegemea nchini kutokuwa kikwazo kwenye utatuzi wa migogoro kwa njia ya usuluhishi.

Akizungumza na Waandishi wa habari mara baada ya kutembelea mabanda ya Mahakama na wadau wake kwenye Maonesho ya wiki ya sheria yanayoendelea katika viwanja vya Nyerere Square jijini Dodoma, Jaji Kiongozi aliwataka Mawakili wa kujitegemea kuwatumikia wananchi kwanza wanapotekeleza majukumu yao

Alisema Mawakili wana nafasi kubwa katika kufanikisha utaratibu huu wa kuamua mashauri kwa njia ya usuluhishi na pia wanayo nafasi kufanikisha usuluhishi hivyo amewataka wasiwe vikwazo.

Jaji Kiongozi alifafanua kuwa Mawakili wa Kujitegemea ni muhimu katika mnyororo wa utoaji haki kwani  wanayo nafasi ya kusaidia upatikanaji wa haki kwa wakati. Aliwakumbusha kuwa pamoja ya kuwa wanayo haki ya kupata kipato lakini wajibu wao wa kwanza ni kuwasaidia wananchi.

Akifafanua kuhusu upatikanaji wa kipato kwa Mawakili na utatuzi wa migogoro kwa njia ya usuluhishi, Jaji Kiongozi alisema katika kazi za sheria, msingi wa kwanza siyo kipato, kipato ni kitu kinachofuata baadaye. Alisema Mawakili wanaweza kutumia usuluhishi na kupata kipato kinachostahili kwa sababu  zipo Sheria zinazoonyesha Wakili anastahili kupata nini kwa shauri la aina gani litakaloshughulikiwa.

Ametoa wito kwa Chama cha Mawakili Tanganyika (TLS) kufanya tafiti kuangalia ushiriki wa Mawakili katika usuluhishi upo kwa kiwango gani na kupitia utafiti huo kuzungumza na wanachama wake ili kuwahamasisha kushiriki moja kwa moja na kufanikisha usuluhishi.

Kabla ya kuongea na Vyombo vya Habari, Jaji Kiongozi alipata fursa ya kutembelea na kukagua mabanda mbalimbali, ikiwemo lile la Jeshi la Polisi, Uhamiaji, Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu, Mamlaka ya Kuthibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya, Mkemia Mkuu wa Serikali, Magereza, Taasisi ya Usuluhishi na Kituo cha Huduma Bora kwa Mteja.

Aidha Jaji Kiongozi alitumia fursa hiyo kuwaalika wananchi wote kwa mara nyingine kufika katika viwanja hivyo  na kupata e;limu kuhusu masuala ya haki.

Maonesho ya wiki ya Sheria yanaendelea katika viwanja vya Nyerere Square jijini Dodoma ambapo Mahakama na Taasisi wadau wa utoaji haki wanashiriki kwenye Maonesho hayo. Maonesho ya wiki ya sheria yatamalizika Januari 29, 2023.