KATIBU WA TUME ATEMBELEA MAONESHO YA WIKI YA SHERIA


  • Atoa Wito kwa wananchi kuzitumia Kamati za Maadili

Na Lydia Churi-Tume ya Utumishi wa Mahakama, Dodoma

Katibu wa Tume ya Utumishi wa Mahakama ambaye pia ni Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante Ole Gabriel ametembelea mabanda ya maonesho ya utoaji wa elimu ya kisheria katika Viwanja vya Nyerere Square jijini hapa na kutoa wito kwa wananchi kuzitumia kamati za Maadili ya Maafisa wa Mahakama kuwasilisha malalamiko yao yanayohusiana na masuala ya nidhamu na maadili.

Prof. Ole Gabriel aliwataka wananchi kuendelea kuuamini Mhimili wa Mahakama kuwa unatenda haki na endapo itatokea kuna tatizo kinyume na matarajio ya Mahakama basi wasisite kuwasilisha malalamiko yanayohusiana na maadili kwenye kamati husika ili hatua stahiki zichukuliwe.

“Tunayo mifumo ndani ya Mhimili wa Mahakama kwa ajili ya kurekebishana kwa kuwa sisi ni binadamu na inaweza kutokea kukawa na baadhi ya watumishi wanaokiuka maadili ya kazi hivyo tumieni kamati za maadili ipasavyo”, alisisitiza.

Alisema zipo kamati za Maadili ya Maafisa wa Mahakama katika ngazi ya Mkoa ambapo Wakuu wa Mikoa ndiyo wenyeviti wa kamati hizo na katika ngazi ya wilaya wakuu wa wilaya ni wenyeviti wa kamati hizo.

Akizungumzia upatikanaji wa haki, Katibu huyo wa Tume ya Utumishi wa Mahakama alisema Mwananchi anapaswa kutambua kwamba pale anapofuatilia haki yake hatua ya awali kabisa ni yeye mwenyewe kuwa na kuhusu sheria ili aweze kujua haki yake ya msingi.

Akimnukuu Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma, alisema hatua ya kwanza kwenye mnyororo wa upatikanaji wa haki ni yule anayetafuta haki kujua sheria inayosimamaia haki yake anayoitafuta.

Alisema pamoja na kuwepo kwa kamati zinazoshughulikia nidhamu na maadili ya watumishi wa Mahakama lakini pia katika eneo la kiutawala, Mahakama  imewekeza kwenye mafunzo kwa kada zote za watumishi ili kuwaelimisha na kuwaelewesha umuhimu wa kutoa huduma bora na nini hasa wananchi wanatarajia kutoka kwao katika suala zima la utoaji haki.

“Tumewekeza zaidi katika kuwaelimisha na kuwaelewesha umuhimu wa maadili ndani ya Mahakama kwa sababu Mahakama ni eneo takatifu, tumejipanga kuhakikisha wananchi wanapata haki kwa wakati”, alisema.

Prof. Ole Gabriel alitumia fursa hiyo kuishukuru Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inayoongozwa na Mhe, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa uwezeshaji mkubwa ambao umechochea uboreshaji wa miundombinu mbalimbali ya Mahakama ikiwemo ujenzi wa majengo ya kisasa.

“Mahakama hatufanyi biashara, kwa hiyo miundombinu yetu inategemea uwezeshwaji kutoka serikalini. Mimi kama Afisa Masuhuli lazima nitoe shukrani kwa Serikali, kwa kweli tunawezeshwa vizuri, tunatumia fedha hizo vizuri na matokeo yanaonekana. Bila uwezeshwaji huo tungekuwa na changamoto kubwa zaidi,” alisema.

Prof. Ole Gabriel akabainisha pia kuwa ujenzi wa Mahakama katika ngazi mbalimbali kama Mahakama za Mwanzo unaendelea kwa kazi kubwa, ambapo Vituo Jumuishi vya Utoaji Haki sita vimeshajengwa mpaka sasa na vingine 12 vitajengwa kufika mwaka 2024, lengo ni kusogeza huduma za utoaji haki karibu na wananchi.

Katibu wa Tume ya Utumishi wa Mahakama alitembelea Maonesho hayo ambapo alipita kwenye mabanda ya wadau mbalimbali wa Mahakama kikiwemo Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto, Bandari, Ofisi ya Mkemia Mkuu wa Serikali, Chuo Kikuu cha Dodoma, Mamlaka ya Kuthibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya, Taasisi ya Kupambana na Kuzuia Rushwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi.