KATIBU WA TUME ATEMBELEA MAONESHO YA WIKI YA SHERIA DODOMA


  • Asisitiza Ushirikiano wa Mihimili na Taasisi za Utoaji Haki

 Na Selina Mlelwa-Tume ya Utumishi wa Mahakama, Dodoma

Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania na Katibu wa Tume ya Utumishi wa Mahakama, Prof. Elisante Ole Gabriel amesema kuwa Mahakama ya Tanzania itaendeleza ushirikiano kati yake na Mihimili ya Serikali na Bunge ili kuwapatia wananchi haki kwa wakati.

Prof. Ole Gabriel ameyasema hayo leo tarehe 27 Januari, 2025 alipotembelea mabanda ya Maonesho ya Wiki ya Sheria yanayoendelea kufanyika katika viwanja vya Nyerere ‘Square’ jijini Dodoma.

Aidha, Katibu wa Tume ametoa rai kwa Taasisi za utoaji haki kushirikiana na Mahakama ya Tanzania katika kuwapatia haki wananchi kwa kuwa ufanisi wa Taasisi hizo ni muhimu kwa utendaji kazi wa Mahakama.

Amewataka Watumishi wa Mahakama nchini kuendelea kuwa sehemu ya maboresho yanayoendelea kufanyika ndani ya Mhimili wa Mahakama na kuunga mkono matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) kwa kuwa ni sehemu muhimu ya maboresho.

Akizungumzia kuhusu Kaulimbiu ya Wiki ya Sheria na Siku ya Sheria ya mwaka huu “Tanzania ya 2050: Nafasi Ya Taasisi Zinazosimamia Haki Madai katika kufikia malengo makuu ya Dira ya Taifa ya Maendeleo,” Prof. Ole Gabriel amesema kuwa, anatarajia kuiona Mahakama mwaka 2050 kuwa ya kifanisi zaidi.

“Ni matarajio yangu kuwa, Mahakama ya 2050 itaendelea kuwa kinara kwa ufanisi, itaendelea kuwa juu zaidi katika ngazi za kimataifa,” ameeleza.

Akiwa katika mabanda hayo, Mtendaji Mkuu wa Mahakam ana Katibu wa Tume  alipata fursa ya kukutana na kuzungumza na watu wenye mahitaji maalum waliofika katika Maonesho ya Wiki ya Sheria kupata elimu kuhusu Mahakama na Sheria kwa ujumla.

Katibu wa Tume alitembelea baadhi ya mabanda ya Wadau wa utoaji haki yakiwemo ya Mahakama ya Tanzania, Mabaraza ya Ardhi ya Wilaya, Chama cha Wanasheria Wanawake Tanzania (TAWLA) na Tume ya Kurekebisha Sheria.

Mabanda mengine yaliyotembelewa ni pamoja na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), Wizara ya Katiba na Sheria, Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali, Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali na Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA).

(Imehaririwa na Lydia Churi)