KATIBU WA TUME AWATAKA WATUMISHI KUWAJIBIKA, KUSHIRIKIANA NA KUTUNZA RASILIMALI


Lydia Churi- Tume ya Utumishi wa Mahakama

Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania na Katibu wa Tume ya Utumishi wa Mahakama Prof. Elisante Ole Gabriel amewataka watumishi wa Tume kuwajibika ipasavyo, kushirikiana na kutunza rasilimali za Serikali.

Akifungua Mkutano wa Baraza la Wafanyakazi wa Tume leo tarehe 23 Aprili, 2025 jijini Dar es salaam, Katibu wa  Tume aliwataka watumishi hao kuzingatia mambo hayo matatu ili Tume iweze kupiga hatua katika kusimamia shughuli za utaoji haki nchini.

”Kila Mtumishi wa Tume anapaswa kuwajibika ipasavyo katika nafasi yake, natamani kila mtu afanye kazi kwa kiwango cha juu kabisa  ili Taasisi yetu iende vizuri na kusonga mbele”, alisema.

Aidha, Katibu wa Tume pia aliwataka watumishi hao kushirikiana na kushikamana licha ya tofauti zinazoweza kuwepo kati yao kwa kuwa ni binadamu na kwamba tofauti hizo hazina budi kuvumiliwa.

Jambo lingine ambalo Katibu wa Tume alilisistiza ni Watumishi hao kutunza rasilimali walizopewa na Serikali likiwemo jengo jipya na la kisasa la Ofisi za Tume lililopo mjini Dodoma, magari pamoja na vifaa vingine vilivyonunuliwa kwa fedha za Serikali.

 Akizungumzia mafanikio ya Tume katika kipindi cha miaka minne y uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan, Prof. Ole Gabriel alisema Tume kama msimamizi wa shughuli za Mahakama ya Tanzania inao wajibu wa kuhakikisha inaboresha mazingira ya kazi kwa watumishi, kuongeza idadi ya watumishi pamoja na kutetea maslahi yao.

Alisema katika kutekeleza majukumu yake, Tume kama chombo kinachomshauri Rais kuhusu uteuzi wa Viongozi mbalimbali wa Mahakama kimekuwa kikiwasilisha mapendekezo ambayo yaliridhiwa na Rais na hivyo kupatikana kwa Viongozi wa Mahakama ya Tanzania.

Alisema kuwa katika kipindi cha miaka minne ya Uongozi wa Rais Mhe. Dkt. Rais Samia, jumla ya Majaji 68 wa Mahakama Kuu ya Tanzania waliteuliwa baada ya Rais kuridhia mapendekezo ya Tume. Kwa sasa idadi ya Majaji wa Mahakama Kuu inafikia takribani Majaji 105.

Alisema katika kipindi hicho cha miaka minne ya uongozi wa Rais Samia  mapendekezo ya Tume yaliwezesha kufanyika kwa uteuzi wa Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mtendaji Mkuu wa Mahakama na Msajili Mkuu wa Mahakama.

Katibu wa Tume aliongeza kuwa Tume katika kuimarisha utendaji wa kazi zake, katika kipindi cha miaka minne imeajiri Watumishi 1,564 ambapo kati yao, 235 ni Maafisa Mahakama (Mahakimu) na 1,239 ni watumishi wasio Maafisa Mahakama.  Aidha, Tume pia iliteua Naibu Wasajili 65, Watendaji wa Mahakama 19, Wakurugenzi 6 na Wakurugenzi Wasaidizi 5.   

Kwa Upande wake, Naibu Katibu wa Shirikisho la vyama vya Wafanyakazi wa Serikali Kuu (TUGHE) Taifa Bw. Ngodo alimpongeza Katibu wa Tume ya Utumishi wa Mahakama kwa jitihada kubwa anazofanya za kuhakikisha Watumishi wa Tume wanafanya kazi Katika mazingira bora na kutetea maslahi yao.

Aidha, aliwashauri watumishi hususan wa ngazi za chini kujiendeleza kielimu ili waweze kupata sifa zitakazowasaidia kupanda ngazi katika Utumishi wao.

Naibu Katibu wa TUGHE Taifa pia ameipongeza Tume ya Utumishi wa Mahakama kwa kuwa na jengo zuri na la kisasa la ofisi ambapo  amesema litahamasisha utendaji kazi kwa kuwafanya watumishi kufanya kazi katika mazingira bora.