KATIBU WA TUME YA UTUMISHI WA MAHAKAMA ATEMBELEA MAONESHO YA SABASABA
Na Mwandishi-Tume ya Utumishi wa Mahakama, Dar es salaam
Katibu wa Tume ya Utumishi wa Mahakama ambaye ni Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante Ole Gabriel leo tarehe 9 Julai, 2024 ametembelea Maonesho ya 48 ya Biashara ya Kimataifa 2024, na kujionea shughuli mbalimbali za uwekezaji zinazofanywa na Wananchi na Taasisi mbalimbali.
Prof. Ole Gabriel aliwasili katika Viwanja vya Sabasaba vilivyopo katika Barabara ya Kilwa, Wilaya ya Temeke katika Mkoa wa Dar es Salaam majira ya saa 5.30 asubuhi na kukutana na Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhe. Dkt. Suleiman Jaffo katika Ofisi za Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania.
Baada ya kupokea taarifa fupi kuhusu maonesho hayo, Katibu wa Tume alipitishwa katika mabanda mbalimbali aliyopangiwa ambayo ni Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, Taasisi Moyo ya Jakaya Kikwete na Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi.
Mabanda mengine aliyotembelea ni Mifuko ya Jamii ya NSSSF na PSSSF, Wizara ya Katiba na Sheria, Wizara ya Mifugo, Mahakama ya Tanzania na Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC).
Akizungumza baada ya kutembelea mabanda hayo, Prof. Ole Gabriel amewapongeza waandaaji wa maonesho hayo ambayo yalifunguliwa na Rais wa Msumbiji, Mhe. Filipe Jacinto Nyusi, akiwa na mwenyeji wake, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan.
“Kwa kweli maandalizi ni makubwa na yamefana. Sikuweza kutembelea mabanda yote, lakini nimeona mwamko mkubwa sana kwenye yale niliyotembelea. Bahati nzuri miaka ya nyuma ya 2001 hadi 2011 nilifanikiwa kuwa mmoja wa Majaji wa Maonesho kama haya. Niliyokuwa nayaona wakati ule na ninayoyaona sasa miaka hii ni mabadiliko makubwa sana,” alisema.
Aidha, alitoa mfano katika banda la Hospitali ya Taifa ya Muhimbili namna uwekezaji mkubwa ulivyofanyika kwenye matibabu ambapo wamefikia katika hatua ya utalii wa kimatibabu, hivyo alimpongeza Mkurugenzi Mkuu Prof. Mohamed Janabi pamoja na Watalaam wengine.
Alitumia fursa hiyo kuipongeza Serikali ya Awamu ya Sita kwa uwekezaji mkubwa katika maeneo mbalimbali yanayoshajirisha maendeleo ya nchi na Watanzania kwa ujumla. Pia alitoa ushawishi kwa Wizara ya Viwanda na Biashara kuendelea kuyapa uzito maonesho hayo kwani yameshavuka mipaka ya Tanzania na ni eneo ambalo watu wanaweza kujitangaza vizuri.
“Kuwa na bidhaa ni jambo moja, lakini kuhakikisha kwamba bidhaa ile imefahamika vizuri kwa jamii na kwenye soko ni jambo la muhimu zaidi. Ndiyo maana kwenye taaluma ya biashara kuna kitu kinaitwa marketing mix na moja wapo ni promotion. Maonesho haya ni moja ya promotion,” amesema.
Prof. Ole Gabriel amewashauri Watanzania kutumia fursa hiyo vizuri siyo tu kuleta kwenye maonesho kuonyesha bidhaa, lakini ubora ni wa muhimu zaidi ili wateja wa ndani na nje waweze kuamini kwamba bidhaa iliyotengenezwa na Watanzania ni bora zaidi.
Amebainisha kuwa mara zote katika huduma au biashara mteja hanunui bidhaa, bali hununua thamani, hivyo ubora katika bidhaa husaidia kuongeza pato la Taifa, hasa pale kila mmoja anapotamani kuuza nje na kuwezesha kupata fedha nyingi za kigeni.
“Rais wetu, Dkt. Samia Suluhu Hassan ametutengenezea mazingira mazuri ya diplomasia uchumi nje ya nchi, lililopo kwetu sisi ni kutumia fursa hii vizuri,” amesema.
Tume ya Utumishi wa Mahakama ni miongoni mwa Taasisi za utoaji haki zinazoshiriki kwenye Maonesho hayo zikiwa na mabanda ndani ya banda la Mahakama ya Tanzania kwa lengo la kutoa huduma na elimu kwenye masuala mbalimbali yanayohusu Sheria kwa ujumla. Maonesho ya 48 ya Biashara ya Kimataifa ‘Sabasaba’ yalianza tangu tarehe 28 Juni, 2024 na yanatarajiwaq kumalizika ifikapo Juni 13, 2024.