MAAFISA TARAFA WATAKIWA KUWAELIMISHA WANANCHI NAMNA YA KUWASILISHA MALALAMIKO


Na Lydia Churi- Tume ya Utumishi wa Mahakama, Arusha

Naibu Katibu wa Tume ya Utumishi wa Mahakama (Maadili na Nidhamu) Bi. Alesia Mbuya ametoa rai kwa Maafisa Tarafa kuwaelimisha Wananchi namna sahihi ya kuwasilisha malalamiko yanayohusu ukiukwaji wa maadili ya Maafisa Mahakama.

Akifunga Mafunzo ya siku mbili kwa Maafisa Tarafa wa Mkoa wa Arusha mwishoni mwa wiki mkoani humo, Naibu Katibu huyo alisema mafunzo waliyopatiwa Maafisa hao na Tume ya Utumishi wa Mahakama yatawawezesha kutekeleza  majukumu yao kuzingatia Sheria, Kanuni na mwongozo pasipo kuingilia jukumu la Mhimili mwingine wa Dola.

 ”Kwa kuwa mafunzo haya yalihusisha mada kuhusu Muundo na majukumu ya Tume, Kanuni za Maadili ya Maafisa Mahakama na Uwasilishaji wa Malalamiko na Mgawanyo wa Majukumu kati ya Mihimili ya Dola, ni dhahiri kuwa yatawsaidia kuwaelisha wananchi namna sahihi ya kuwasilisha malalamiko yao yanayohusu ukiukwaji wa maadili ya Maafisa Mahakama”, alisema.

Alisema kuwa msingi wa mafunzo hayo ni Mkakati wa Tume ya Utumishi wa Mahakama wa kuwafikia wananchi na kutoa elimu kuhusu uwepo wake, namna inavyotekeleza majukumu yake zikiwemo kamati zinazopokea malalamiko ya ukiukwaji wa maadili kwa Maafisa Mahakama na namna ya kuwasilisha malalamiko hayo.

Naibu Katibu huyo alisema moja ya mikakati ya Tume ni kuwaelimisha Maafisa Tarafa wa Mkoa wa Arusha ili nao wakawaelimishe wananchi pale wanapotekeleza majukumu yao ya kila siku, kwa kuwa Maafisa Tarafa ni kiungo muhimu kati ya Serikali na Wananchi katika Tarafa.

Alimshukuru Jaji Mkuu wa Tanzania na Mwenyekiti wa Tume ya Utumishi wa Mahakama Prof. Ibrahimu Hamis Juma pamoja na Makamishna wote wa Tume kwa kuridhia kufanyika kwa mafunzo hayo ambayo yatawezesha upatikanaji wa haki kwa wananchi. 

Aidha, Naibu katibu pia aliwashukuru Maafisa Tarafa kwa kuona umuhimu wa mafunzo hayo na kuacha shughuli zao kufika kwenye mafunzo hayo. Aliahidi kuwa Tume itaendeleza ushirikiano na Maafisa Tarafa ili kuwahudumia wananchi.

Tume ya Utumishi wa Mahakama iliandaa mafunzo ya siku mbili kwa Maafisa Tarafa wa Mkoa wa Arusha kwa lengo la kuwaelimisha  kuhusu Kanuni na Miongozo ya Kamati za Maadili za Maafisa Mahakama ili nao wakawaelimisha wananachi uwepo wa Kamati hizo na namna ya kuwasilisha malalamiko yanayohusu ukiukwaji wa Maadili ya Mahakimu.