MABADILIKO YA KIFIKRA NA KIMTAZAMO YAIWEZESHA MAHAKAMA KUFIKIA MAFANIKIO
Na Lydia Churi- Tume ya Utumishi wa Mahakama, Dodoma
Jaji Mkuu wa Tanzania na Mwenyekiti wa Tume ya Utumishi wa Mahakama Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma amesema mabadiliko ya kifikra na kimtazamo yameiwezesha Mahakama ya Tanzania kutekeleza Dira ya Taifa ya Maendeleo ya mwaka 2025 na kufikia mafanikio katika uboreshaji wa huduma zake.
Akizungumza wakati wa Sherehe za Maadhimisho ya Siku ya Sheria nchini zilizofanyika leo tarehe 3 Februari 2025 kwenye Viwanja vya Chinangali jijini Dodoma, Jaji Mkuu alisema maboresho endelevu yanahitaji kubadili mitazamo na tamaduni katika utoaji wa huduma hususan za utoaji haki.
Alisema hivi sasa watumishi wa Mahakama wanafanya kazi kwa kuleta matokeo yanayopimika na kwa kuzingatia weledi.
“Watumishi wa Mahakama wanafanya kazi kwa ushirikiano, mawasiliano na kwa mashauriano, utumishi wa Mahakama unalenga kutoa huduma zinazowaridhisha wadau, wadaawa na wananchi wote wanaofuata huduma za Mahakama.”, alisema.
Akizungumzia utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo ya mwaka 2050, Jaji Mkuu alisema katika kuelekea Tanzania yam waka 2050, Taasis za hakimadai zinayo nafasi ya kipekee katika kuhakikisha malengo ya maendeleo ya Taifa yanafikiwa.
Alizitaja Taasisi hizo kuwa ni Mahakama ya Tanzania, Kituo cha Sheria naHaki za Binadamu, Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali, Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Wakala wa Usajili Ufilisi na Udhamini (RITA), Wizara ya Katiba na Sheria, Tume ya Kurekebisha Sheria, Chama cha Mawakili Tanganyika (TLS), na Taasisi nyingine zinazohusika na hakimadai pamoja na wananchi wote.
Alisema kuwa kufikiwa kwa malengo ya Dira ya mwaka 2050 kutategemea mabadiliko makubwa yatakayofanywa ndani ya taasisi zinazosimamia hakimadai ili ziwezeshe Tanzaniakufikia maono na dhamira ya kuwa nchi ya Uchumi wa kipato cha kati ngazi ya juu.
Aidha, Mwenyekiti wa Tume alimshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan na Serikali kwa kuiwezesha Mahakama kufikia mafanikio hasa kwa kuwezesha kupitia fedha za ndani pamoja na za wahisani.