MABORESHO YA KANUNI YALIYOFANYWA NA MAHAKAMA YA TANZANIA YAIMARISHA UTOAJI HAKI


Na Mwandishi-Mahakama, Morogoro

Maboresho yaliyofanywa na Mahakama ya Tanzania kwenye kanuni mbalimbali za uendeshaji wa mashauri yameleta matunda yaliyokusudiwa, ikiwemo kuongeza imani kwa umma, uwajibikaji wa watumishi na kuharakisha jukumu la utoaji haki kwa wananchi.

 Hayo yamesemwa na Mkurugenzi wa Usimamizi wa Mashauri wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. Desdery Kamugisha wakati akizungumza katika mkutano wa kila mwezi wa vyombo vya habari, uliofanyika tarehe 31 Oktoba, 2024 kwenye ukumbi wa mkutano wa Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki(IJC), Morogoro, kuhusu mchango wa maboresho ya kanuni za mahakama katika upatikanaji wa haki kwa wakati.

Amebainisha kuwa utafiti uliofanywa na Taasisi huru ya FKL Associates Advocate kuhusiana na kuanzishwa kwa kanuni 20 katika Mahakama ya Tanzania umeonesha kwamba asilimia 79.1 ya wananchi wote nchi nzima waliohojiwa wameridhika na marekebisho ya kanuni za mwenendo wa mashauri ya madai kwa kupunguza hatua za shauri kutoka 28 hadi 21.

“Utafiti huo uliofanyika mwezi Aprili, 2024 umeonesha kuwa, kwa ujumla wananchi wameridhika kwamba kanuni hizi imeongeza upatikanaji wa haki kwa wakati, uwazi, ubora wa upatikanaji wa haki na ufanisi,” Mhe. Kamugisha amesema.

Amebainisha kuwa, pamoja na mambo mengine, Taasisi hiyo ilifanya tathimini kwenye matokeo ya kanuni katika kuboresha utoaji haki, hasa kupunguza muda na gharama za kuendesha mashauri, kuboresha ubora wa haki, kuongeza ufanisi na uwazi kupitia matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano(TEHAMA) na kuongeza wigo wa haki kwa  makundi yaliyo hatarini na mazingira magumu.

Aidha, Mhe. Kamugisha amesema asilimia 86.8 ya wananchi walihojiwa kwa ujumla wamesema kanuni zinazoruhusu ufunguaji wa mashauri na usikilizaji kwa njia ya  mtandao zimeongeza kasi ya usikilizaji  wa mashauri na kupunguza muda wa mashauri wa kukaa mahakamani. 

Katika matokeo ya ujumla taarifa hiyo inaonesha kwamba asilimia 86.8 ya wananchi waliohojiwa wamekubali kuwa kanuni zimepunguza gharama za kuendesha wa mashauri na asilimia 88.8 ya wananchi walihojiwa wamesema kanuni zimeboresha mazingira ya usuluhishi,” alisisitiza. 

Mhe. Kamugisha amefafanua kwamba ripoti hiyo inaonesha asilimia 64 ya wananchi wamekubali matumizi ya TEHAMA yameongeza uwazi, kwani maamuzi ya Mahakama ya Rufani Tanzania na Mahakama Kuu ya Tanzania yanapatikana kwenye TanzLII, huku maamuzi ya mahakama za chini yakipatikana katika maktaba mtandao.

Amebainisha kuwa kabla ya kanuni hizo mlundikano wa mashauri kwa mwaka 2020 ulikuwa ni asilimia 15, lakini baada ya kanuni hizo kutoka, mlundikano umeendelea kupungua ambapo kwa mwska 2021 ilikuwa asilimia 10.9, mwaka 2022 ikawa asilimia sita, mwaka 2023 imekuwa asilimia tano na mwaka 2024 hadi mwezi Septemba ni asilimia tatu.

Halikadhalika, Mhe. Kamugisha amesema wastani wa muda wa kusikiliza shauri mahakamani kwa mwaka 2021 ulikuwa siku 119, mwaka 2022 ni siku 95 na mwaka 2023 siku 84, hivyo kasi ya usikilizaji na uondoshaji wa mashauri imeongezeka.

Ameeleza kwamba kwa kipindi cha 2020 hadi 2024 pekee, kanuni mpya 12 zimetungwa na tatu kurekebishwa. Idadi hiyo haiushishi kanuni mbalimbali zilizoanzisha Mahakama za Hakimu Mkazi (RM) na Mahakama za Wilaya (DC) na masjala za Mahakama za Mahakama ya Rufani na Mahakama Kuu katika mikoa mbalimbali.

Maboresho mengine ya kikanuni yaliyofanywa ni Mahakama kumrahishia mjasiliamali mdogo kwa kuondoa taratibu za kiufundi kwa mashauri yasiozidi milioni 100 kusikilizwa kwenye Mahakama ya Hakimu Mkazi na kumalizika katika kipindi kisichozi miezi sita.